Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yaanza kushughulikia changamoto zinazowakabili Mawakili wa Serikali nchini

NA DIRAMAKINI

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kushughulikia changamoto zinazowakabili Mawakili wa Serikali nchini.
Ameyasema hayo leo Desemba 6,2024 mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe. Palamagamba Kabudi ambaye alikuwa anafungua kikao kazi cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakurugenzi wa Divisheni zikiwemo Idara na Wakuu wa Vitengo vya Sheria Serikalini.

"Na tayari Serikali ilitoa waraka na posho kwa Mawakili wa Serikali ambapo kwa sasa kupitia waraka huo mawakili wanaweza kulipwa posho za mavazi ya mahakama, ada ya vyama vya kitaaluma, ada ya Kamishna wa Viapo na gharama za kuhudhuria mafunzo endelevu ya kitaaluma."

Kikao kazi hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya maeneo Mawakili hawalipwi.
"Na kama nilivyotangulia kuwasilisha pale mwanzo tunaomba sana mlifanyie kazi ili waweze kuwa vizuri."

Pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria iwaongezee bajeti katika ofisi hiyo.

"Ili tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri. Mheshimiwa mgeni rasmi (Waziri Kabudi) kwa muda mfupi niliohudumu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini na kama mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali nimefahamishwa au kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi na Mawakili wa Serikali ya kutoruhusiwa na waajiri wao kwenda kwenye mikutano au shughuli za Chama cha Mawakili wa Serikali.

"Nitumie fursa hii kumuomba Katibu Mkuu tena wa Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hii kupitia vikao vyenu ili Mawakili wa Serikali waweze kuruhusiwa kushiriki kwenye shughuli za chama."

Amesema, chama hicho kilipata bahati ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan mwezi Septemba,2022.
"Lakini, (Mheshimiwa Rais Dkt.Samia) alienda mbali zaidi na kutanguliza ufadhili kwa miaka ile ya mwanzo, hii inaashiria nini?.

"Hii inaashiria kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana lengo la kuhakikisha kwamba chama hiki kinakuwa imara.

"Lakini, hakiwezi kuwa imara kama baadhi ya wanachama hawaruhusiwi kushiriki shughuli za chama hiki."

Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 16A(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura 268 na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti 2019.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news