MBEYA-Watu watano wa familia moja wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakiwa wamelala kwenye kambi ya kuchungia ng’ombe wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.
Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Balaa Scania (39) ambaye ni mfugaji,Kulwa Luweja (17),Masele Masaganya (16),Hema Tati (10) na
Manangu Ngwisu (18).
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 29, 2024 likiwahusisha wakazi hao wa Kitongoji cha Nkangi kilichopo Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, watu hao walifariki dunia baada ya mvua kubwa iliyonyesha usiku ikiwa imeambatana na radi.
Amesema,watu hao walikuwa wamelala kwenye kambi ya kuchungia ng'ombe wakati walipopigwa na radi na walifariki dunia papo hapo.
Kamanda Kuzaga alisema kuwa, watu watano wengine walijeruhiwa na walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana kwa matibabu zaidi.
Majeruhi hao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya (13), Seni Solo (13), Paskali Kalezi (16) na Huzuni Kalezi (19).
"Walitibiwa na hali zao zilikuwa nzuri, hivyo waliruhusiwa kurejea nyumbani."