ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za muhimili wa Mahakama zenye lengo la kuleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya majengo yake.
Ameyasema hayo leo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza, Serikali imefanikiwa kuleta mageuzi makubwa kwenye majengo ya Mahakama kwa kutoa fedha za ndani kwa asilimia 100 jambo alilolieleza kuwa la kujivunia.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema, mageuzi hayo yana lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi katika mazingira ya kuridhisha hatua aliyoielezea kwamba itaijengea heshima muhimili huo.
“Tumetumia fedha zetu wenyewe kwa sababu tungetumia wafadhili tungechelewa kufikia mafanikio haya,”amebainisha Rais Dkt.Mwinyi.
Akilizungumzia jengo la zamani la Mahakama ya Vuga, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza litaendelea kuwa la Mahakama na kuridhia azma ya Mahakama ya kulifanya jengo hilo kuwa Makumbusho ya Mahakama.