ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, ameuagiza Mfuko wa Barabara kuzifanyia ukarabati barabara mpya zote mara tu zitakapopata hitilafu kwa kuzitengeneza na kuzipaka rangi ili kuzirejesha kwenye haiba yake.Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa barabara ya kilomita 6.5 inayotoka Uwanja wa Ndege, Wilaya ya Magharibi B hadi Mnazi Mmoja Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi iliyopewa jina la Uwanja wa Ndege-Kiembesamaki.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameiasa jamii kutozitumia njia za wapita kwa miguu kinyume na makusudio yaliyowekwa na Serikali, kufanya hivyo ni kosa la matumizi ya barabara hizo.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amezitaka mamlaka zinazosimamia hifadhi ya barabara kuendelea kuwaelimisha wananchi wasijenge karibu na hifadhi ili kuinusuru Serikali kubeba mzigo mkubwa wa kulipa fidia inapotaka kupitisha miundombinu ya jamii ikiwemo kuzitanua barabara hizo na kupitisha huduma nyengine za mawasiliano.
Katika hatua nyingine Rais Dkt.Mwinyi ameridhia maombi wa wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kuwekewa taa za barabani kwenye ujenzi wa barabara yao ya kwanza inayojengwa kisiwani humo kwa nguvu za Serikali.