ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Chuo Kikuu cha Zanzibar kimemtunuku Shahada hiyo ikiwa ni kutambua na kuthamini Mchango wa Uongozi wake Unaoacha Alama na historia itakayokumbukwa wakati wote.
Hafla ya kutunukiwa Shahada hiyo imefanyika leo tarehe 5 Disemba 2024 katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu wakati wa Mahafali ya 22 ya Wahitimu wa mwaka 2024.
Shahada hiyo ya Heshima ya Uchumi ametunukiwa kuthamini mchango wake na mafanikio makubwa yaliofikiwa Zanzibar hususan Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo yaliopatikana Kipindi kifupi cha Uongozi wake wa miaka minne akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Rais Dkt.Mwinyi amekishukuru chuo hicho kwa kuthamini juhudi na kazi anazofanya kwa ajili ya Maendeleo ya nchi.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa Shahada hiyo aliotukuwa inaakisi kazi nzuri inayoifanya na Serikali anayoiongoza na itamuongezea hamasa ya maendeleo zaidi.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi ameahidi kuienzi heshima hiyo na kuwahakikishia wananchi kuendelea kuwatumikia kwa uwezo wake wote na sio mwisho wa safari bali mwanzo wa hatua kubwa ya maendeleo yajayo.