Rais Dkt.Mwinyi awashukuru madaktari kutoka India

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewapongeza na kuwashukuru madaktari kutoka Hospitali ya MIOT ya India kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia Wazanzibari hasa wagonjwa wa moyo, saratani na kiharusi.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 11,2024 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na uongozi wa hospitali hiyo ya MIOT ya Chinnai, India wakiongozwa na mwenyeji wao Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wakuu wa Wizara ya Afya, Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza pia uhusiano mzuri uliopo baina ya hospitali hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na kueleza kuwa kuwepo kwao kumeongeza tija kubwa kwa jamii ya Wazanzibar wenye mahitaji ya huduma zao.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameleeza kuwa Serikali imekua ikitumia gharama kubwa kufuata baadhi ya matibabu nje ya nchi hasa kwa wagonjwa wa moyo jambo alilolieleza haliathiri tuu wagonjwa bali na jamaa wa wagonjwa hao wanaoambatana nao wakati wa matibabu.

Ameeleza kuwepo kwa madaktari hao nchini, ni fursa nzuri kwa wataalamu wa ndani kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo, utaalamu pia kupunguza gharama kubwa kwa wagonjwa wanaopata matibabu kutoka taasisi hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa hospitali hiyo ya MIOT, Dkt. Prithvi Manawng Mohandas amemueleza Rais Dk. Mwinyi huduma wanazozitoa kwa wagonjwa wa Zanzibar hasa kwa maradhi ya saratani ni tiba za mionzi (Redio therapy), matibabu ya kikemia (Chemical Therapy) na tiba ya kulenga eneo maalum (targeted therapy) pamoja na matibu ya moyo.

Akizungumzia ugonjwa wa kiharusi Dk. Prithvi amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba wanawatibu wagonjwa wa maradhi hayo hasa kwa kuwasaidia kuimarisha na kurejesha uwezo wa viungo vyao kwa kutembea na kufanya shughuli zao za kawaida kwa maisha yao ya kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news