NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wafanyakazi wote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kasi ya kuharakisha maendeleo kwa ustawi bora wa Taifa na wananchi.
"Wito wangu kwa wafanyakazi wote ni tuazimie kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa bidii mwaka 2025, kila mmoja kwa nafasi yake, ili kufanikisha jitihada zetu za kuleta maendeleo;
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 30,2024 kupitia hotuba yake kwa umma ya kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025.
"Katika siku kama ya leo, tumekuwa tukiendeleza utaratibu wa kueleza japo kwa muhtsari matukio makubwa ambayo nchi yetu imeyapitia na kutakiana heri na baraka za mwaka tunaoukaribisha.
"Tunapoungana na wananchi wa mataifa mbalimbali duniani katika kuuaga mwaka wa 2024 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025 tunao wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa katika nchi yetu.
"Kwa hakika, kutokana na misingi hiyo nchi yetu imeweza kupata mafanikio makubwa katika jitihada zetu za kukuza uchumi, kuimarisha miundombinu, biashara na uwekezaji, huduma za kijamii na kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora."
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, nchi imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kukuza uchumi mijini na vijijini.
"Tumepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi na kudhibiti ukusanyaji wa mapato na kuimarisha uwekezaji na biashara."
Pia, amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika ujenzi wa miundombinu ya barabara mijini na vijijini, viwanja vya ndege na bandari.
Ujenzi wa nyumba za makazi, usambazaji wa huduma za umeme na huduma za maji safi na salama pamoja na uimarishaji wa sekta ya elimu na afya kote nchini.
"Aidha, tumefanikiwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuanzisha programu za utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa makundi ya wananchi na kuwajengea mazingira bora ya kufanya biashara hasa baada ya kufunguliwa rasmi kwa masoko makubwa na ya kisasa ya Mwanakwerekwe na Jumbi."
Vilevile Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, wanakamilisha mwaka 2024 ikiwa wamepiga hatua kubwa katika sekta ya michezo kwa mafanikio.
"Baada ya kufanya ukarabati mkubwa wa Viwanja vya michezo vya Amani Complex pamoja na Gombani, jitihada ambazo zimekwenda sambamba na ujenzi wa viwanja vya michezo mbalimbali pamoja na Hoteli ya Amani.
"Jitihada hizi, zinalenga kuimarisha sekta ya michezo na kuchochea shughuli za utalii kupitia michezo na matamasha."
Mbali na hayo Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,"Tunapokamilisha mwaka huu wa 2024, ahadi yangu kwa wananchi ni kwamba Serikali itaendelea kudumisha amani tuliyo nayo.
"Kutokana na umuhimu wa kuadhimisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 katika historia ya nchi yetu, napenda kutoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya sherehe hizi.
"Hii ni hatua ya kuonesha uzalendo na kuthamini jitihada za waasisi wetu na kufanya mapinduzi ili kuikomboa nchi yetu."
Tazama hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi hapa;