ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga uwanja mwingine mkubwa wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa, utakaotumika kwenye michuano ya AFCON, mwaka 2027.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa viwanja vipya vya michezo Maisara (Maisara Sports Complex), Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza Serikali imelenga kujenga viwanja vya kisasa vya michezo kila wilaya pamoja na Sports Academy kila Mkoa.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inakusudia kufanya marekebisho makubwa ya viwanja vya Gombani Kisiwani Pemba na Uwanja wa Mao Tse Tung, Unguja lengo ni kuwa na viwanja vya kisasa vyenye hadhi vitakavyokuwa chachu ya kuwainua vijana kimichezo.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amesema Zanzibar ina nia ya kurudi tena kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) hivyo ujenzi wa viwanja hivyo ni chachu itakayoleta ushawishi wa kupata uanachama huo.