ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuandaa mikakati maalum itakayovutia na kuleta mashindano ya michezo mbalimbali nchini ili viwanja vilivyojengwa kutumika ipasavyo.
Rais Mwinyi ameyasema hayo alipozindua awamu ya pili ya Uwanja wa Amani Sports Complex Mkoa wa Mjini Magharibi, uliojumuisha miradi mbalimbali ikiwemo hoteli inayokaribiana na hadhi ya nyota tano.
Pia, mgahawa wenye hadhi ya kimataifa, maegesho ya magari, maduka na viwanja mbalimbali vya michezo (In door games) ya Judo, Ngumi, mpira wa kikapu (basketi ball), mpira wa wavu, (volleyball).
Vilevile,mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa “long tennis”, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amehimiza kutumiwa kwa kumbi za mikutano zilizomo kwenye uwanja huo kwa mikutano ya ndani na ya kimataifa pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuzitumia fursa zinazopatikana viwanjani hapo kwa kushiriki michezo hiyo kwa lengo la kujiongezea tija na kukuza sekta ya michezo nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Zanzibar ina kila sababu ya kujivunia kwa kuwa na viwanja bora vyenye viwango vya kisasa vya kimataifa.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeiweka Zanzibar kwenye viwango vya kimataifa, hasa linapokuja suala la michezo kwamba itazidi kujibebea hadhi ya kimataifa kwa kuwa na viwanja vyenye hadhi ya juu kila eneo.
Hafla ya uzinduzi huo wa awamu ya pili ya Uwanja wa Amani Sports Complex, iliambatana na pongezi maalum pamoja na keki iliyoandaliwa na Wanafunzi wa Skuli za Maandalizi, Msingi na Sekondari katika kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa katika viwanja vya Amaan, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 23 Disemba 2024.