DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameishauri Bodi mpya ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa kuhakikisha inaendelea kuwa chombo cha kuaminika na Watanzania kwenye kuimarisha sekta ya afya ndani na nje ya nchi kama ilivyo Dira ya taasisi hiyo.Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 14,2024 alipozindua Bodi Mpya ya BMF katika hafla iliofanyika Ukumbi wa BMF Kawe jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt.Mwinyi ambae ni Msarifu wa taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ameeleza kuwa ni vema kwa sifa za wajumbe wa taasisi hiyo kuendelea kudumu ndani ya taasisi ili kuwavutia washirika zaidi na kuhakikisha ukuaji endelevu wa kuwahudumia walengwa wa taasisi hiyo.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa Mpango Mkakati wa Taasisi hiyo utakaodumu kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2030 utategemea Bodi na Menejimenti katika kutekeleza na kufikia malengo yaliowekwa na kusisitiza umuhimu wa kudumisha rekodi nzuri ya utawala Bora, Uongozi mahiri, Utendaji wa kazi wa taasisi hiyo.
Rais Dkt.Mwinyi ambae pia ni Msarifu wa BMF amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa "Imara Horizon Company", Balozi John Ulanga na wajumbe wenzake kwa kufanikisha Ujenzi wa Jengo la "Mkapa Health Plaza" kwa kipindi cha miezi 12 tangu alipoweka jiwe la Msingi Julai 2023.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti Mpya wa BFM Balozi, Liberata Mulamula ameahidi kwa bodi hiyo kufanya kazi kwa karibu na Serikali zote mbili za SMT na SMZ katika kufikia malengo na Dira ya taasisi hiyo.
Rais Dkt.Mwinyi amekabidhi vyeti maalum vya Ushirikiano na Shukrani kwa Wajumbe wa bodi ya BMF waliomaliza muda wao pamoja kukabidhi nyaraka muhimu kwa Bodi Mpya kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo Ripoti maalum ya miaka mitano.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa Bodi mpya ya BMF pia ilihudhuriwa na Mjane wa Hayati Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa.