ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga kituo cha kisasa cha mabasi ya abiria, pembezoni mwa maegesho ya magari Malindi, sambamba na ujenzi wa kituo kikubwa cha magari ya abiria pamoja na uwanja wa michezo kwa vijana.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua maegesho ya magari ya kwanza ya ghorofa Malindi Zanzibar, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi amesema,Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mingine mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa ukiwemo mradi wa taxi za baharini ambapo ujenzi wa bandari za teksi hizo umeanza Maruhubi.
Ni teksi zitakazosafirisha na kushusha abiria watakaotumia usafiri wa majini ikiwemo ujenzi wa treni zitakazotumia barabara za lami kutoka Malindi Mjini hadi Bububu.
Vilevile,ujenzi wa barabara nne za juu zenye mapishano pamoja na ujenzi wa jeti kwa usafiri wa baharini kuwasafirisha watalii wanaotembelea visiwa vidogovidogo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kutekeleza wajibu wao wa kutoa mafao kwa wananchi kwa wakati na kwa kiwango kizuri.
Sambamba na kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kufanikiwa kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi kwa kujenga miradi mikubwa, akitolea mfano mataifa mengine duniani kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ndio inayojenga nchi, hivyo aliitaka ZSSF kuendeleza utaratibu huo.