Rais Dkt.Samia ameagiza fedha za Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru zielekezwe kutoa huduma za kijamii-Waziri Mkuu

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Mwaka 2024 yafanyike katika ngazi ya mikoa na Fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya Maadhimisho hayo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii.
Amesema kuwa kila mkoa uhakikishe Wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile kwenye Masoko, Hospitali, Kambi za wazee na wenye mahitaji maalum, mashindano ya michezo mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu ambayo nchi yetu imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.

Amesema hayo leo Desemba 04, 2024) katika kikao kazi cha Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. “Sherehe za Mwaka huu hazitakuwa na Gwaride na Shughuli nyingine za Kitaifa”.
Amesema kuwa Serikali inatoa wito kwa Wananchi kushiriki katika shughuli hizo ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru wetu.

“Ninatoa rai kwa Wakuu wote wa Mikoa ya Tanzania Bara, kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo Mahsusi yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha Maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu.”

Ameongeza kuwa shughuli za Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ya Mwaka 2024 zilishaanza tangu tarehe 02 na zitafanyika mpaka tarehe 09 Desemba, 2024 Siku ya kilele.
"Katika Maadhimisho haya, Taasisi zote za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama zinaelekezwa kuhakikisha Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara yanapambwa kwa vitambaa vya rangi ya Bendera ya Taifa, picha rasmi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni Muasisi wa Uhuru wetu pamoja na picha ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ni: Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara: “UONGOZI MADHUBUTI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI NI MSINGI WA MAENDELEO YETU.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news