NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda tume mbili ambapo Tume ya kwanza itafanya tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya pili itaangalia utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kutoka eneo la Hifadhi hiyo huu ukiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa alipokutana na Viongozi wa kimila wa jamii ya kimasai wanaoishi eneo la Hifadhi la Ngorongoro.
Rais Dkt. Samia ameunda Tume ya Rais ya kutathmini kuhusu Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumteua Jaji wa Mahakama ya Rufani Dkt. Gerald Ndika kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wajumbe wa Tume walioteuliwa ni Philemon Luhanjo ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu,, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Zakia Hamdani Meghji , Jaji George Mcheche Masaju ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mshauri wa Rais, Sheria.
Wengine ni Dkt. Richard Muyungi ambaye ni Mshauri wa Rais, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Balozi Salome Sijaona ambaye ni Balozi na Katibu Mkuu Mstaafu, Prof. Wilbard Kombe ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu Ardhi,
Prof. Emmanuel Luoga ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mollel James Moringe ambaye ni Diwani na Katibu wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro pamoja na Moi Aprakwa Sikorei ambaye ni Diwani na Mkazi wa Ngorongoro.
Kwa upande wa Tume ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Rais Dkt. Samia amemteua Mhandisi Musa lyombe, Katibu Mkuu Mstaafu kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wajumbe walioteuliwa ni Sihaba Nkinga ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu, Alphayo Kidata ambayr ni Mshauri wa Rais, Uwezeshaji Biashara na Masuala ya Kodi, Balozi Valentino Mlowola ambaye ni Balozi Mstaafu na aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Balozi Mohamed Mtonga ambaye ni Balozi mstaafu na aliwahi kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali,
Balozi George Madafa, Balozi mstaafu, Haruna Masebu ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Edward Maura Nduleti ambaye ni Diwani na Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro na Bi. Rehema Moisare, Mwalimu na Mkazi wa Ngorongoro.