ARUSHA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuunda tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro mkoani Arusha.
Pia amesema, tume nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamaji kwa hiari kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongo.
Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Desemba 1,2024 katika Ikulu ndogo jijini Arusha wakati akizungumza na viongozi wa Kimila wa Jamii ya Kimasai (Malaigwanani) wanaoishi katika eneo la Ngorongoro.
Amesema,mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya serikali yanayohusu eneo la Ngorongo.
“Ninwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongo (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hii,” amesema Dkt.Samia.
Amesisisitiza kuwa, kuna ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji wa miradi inayopita kwenye maeneo yao.
Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye serikali inayowahudumia watanzania wote.
Hata hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongo.