KATAVI-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku, ambapo inatarajia kugawa mitungi 9,765 katika Mkoa wa Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko leo tarehe 19 Desemba, 2024 ameupokea rasmi mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi kwa Wananchi wa mkoa wa Katavi.
REA, imeingia mkataba na mtoa huduma; kampuni ya Taifa Gas, kampuni ambayo, itahudumia wilaya 3 za Mkoa wa Katavi kwa kuuza mitungi hiyo ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 pamoja na vifaa vyake, katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amewaomba REA kuhakikisha kuwa teknolojia za nishati safi ya kupikia, zinapatikana kwa wakati na kuwafikia Wananchi muda wote ili kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanakuwa endelevu.
Mhe. Mrindoko ameongeza kuwa mkoa unaendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi na amewapongeza Wadau mbalimbali (Wakiwemo REA) wanaosaidia kampeni hiyo kwa kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi.
“Mradi huu unakwenda sambamba na malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034; uliozinduliwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na salama,”amesema RC Mrindoko.
Mtaalam wa jinsia na Nishati kutoka wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt Joseph Sambali, amesema kuwa mitungi ya gesi 9,765 itakayosambazwa mkoani Katavi itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi na salama.
"Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti."