NA LWAGA MWAMBANDE
IKUMBUKWE kuwa,ndoa ni muungano kati ya watu wawili kwa maana ya mke na mume ambao unaokubaliwa na kuheshimiwa na jamii.

Mbali na hayo unaweza kurejea katika baadhi ya maandiko matakatifu kutoka katika Biblia ikiwemo, Mwanzo 2:24 neno la Mungu linasema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Waefeso 5:25 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;
Waefeso 5:33 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe;
Mithali 5:18 “…. Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.
Waefeso 4:2 “kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; 3 na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani”.
Marko 10:9 “Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe;
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.Endelea;
1:Akununulie wigi, usimtose mumeo,
Ajifanye kwako bigi, hizo chipsi zake leo,
Moyoni anzisha vagi, usishushe chako cheo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
2:Tafuna chipsi zege, ambazo wapewa leo,
Usiende cheza rege, zile za kimapokeo,
Kwamba uwe kivuruge, kinyume chake mumeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
3:Kweli inawezekana, amekukera mumeo,
Au mmevurugana, aliyoyafanya leo,
Ni vema kutulizana, kesho wala siyo leo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
4:Kumbuka mazuri mengi, anayofanya mumeo,
Mmeishi siku nyingi, na mna maendeleo,
Huyo kwako ni msingi, hata akichacha leo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
5:Duara dunia yetu, ya jana siyo ya leo,
Neema hufika kwetu, kama kwa upendeleo,
Kuchacha nako ni kwetu, maishani matokeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
6:Mke unao wajibu, wa Neno si mapokeo,
Nyumba yako kuratibu, mpate maendeleo,
Lakini ukiharibu, hapo wakosa upeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
7:Wewe kwa mume mlinzi, kesho jana hata leo,
Ndivyo wanogesha penzi, ndoa inapanda cheo,
Usiyumbe kama mwanzi, uwe kama kipepeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
8:Mume kapewa kupenda, hicho ndicho chake cheo,
Mke acha kumponda, asipofika upeo,
Wajibu ni kumlinda, kila iitwapo leo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
9:Mke kazi kumtii, ukijua ni mumeo,
Sasa vipi humtii, unaachia komeo,
Hivi Neno husikii, ambalo lanenwa leo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
10:Tapeli barabarani, huyo hanao upeo,
Ngetaka cha uvunguni, ngekuja kwenu si leo,
Sasa uko kivulini, anakitoa mumeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
11:Usidanganywe na vitu, hivyo vyote matokeo,
Pengine hamna vitu, hiyo ni hali ya leo,
Mungu siyo wa kwao tu, tawapa maendeleo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
12:Pia kwako mwanamume, sikia ujumbe leo,
Asiye mke ukome, kumfwata mwisho leo,
Umeoa usimame, na huyo huyo mkeo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
13:Na kama haujaoa, siruke kama kipepeo,
Mali zako unatoa, kwa haraka matokeo,
Vema sana ukioa, upate maendeleo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
14:Ndoa na iheshimike, kwani huyo ni mumeo,
Pakulala pasafike, kwani huo ni mkeo,
Mwinginewe asifike, ayafanye maoteo,
Kama upo kwenye ndoa, iheshimu ndoa yako.
(Yeremia 31:22, Mithali 14:1, Waefeso 5:22-23)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602