Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuijengea mazingira mazuri Ofisi ya CAG-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza juhudi za kuijengea mazingira mazuri Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili itekeleze vizuri kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo, ukumbi wa Ziwani Polisi Zanzibar kwenye maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imefanikiwa kuisaidia Serikali kutekeleza kwa ufanisi malengo na mipango yake, na kuongeza kuwa Maendeleo makubwa yaliyofikiwa Serikalini yanatokana na mchango wa udhibiti na ukaguzi bora wenye kuzingatia uwajibikaji, nidhamu na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma nchini.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi amesema, miongoni mwa faida zinazopatikana kwenye Ofisi ya CAG ni pamoja na kusaidia kuongeza Pato la Serikali ambapo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti yake ya kila mwaka, huishauri Serikali juu ya mbinu bora za kuziba mianya ya upotevu wa makusanyo ya mapato ya Serikali, kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuwepo kwa usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali nyengine zimeimarisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za jamii, viwanja vya michezo na masoko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news