ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Mhe. Harusi Said Suleiman amesema, Serikali itaendelea kuboresha, kuhifadhi na kuyafufua maeneo ya Mji Mkongwe ili kukuza hadhi ya urithi wa kidunia na Utalii Zanzibar.
Ameyasema wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa uimarishaji wa Bustani ya "African - House" iliyopo Shangani Mjini Magharib Unguja, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuyafufua maeneo ya Mji Mkongwe ambayo yalipewa hadhi ya kuwa urithi wa dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO mnamo mwaka 2000 ili kuendeleza biashara ya Utalii pamoja na Kudumisha utamaduni wa Mzanzibar.
Aidha, Waziri Harusi amesema ili kuyafikia mikakati hiyo jamii inapaswa kuyatunza maeneo haya kwa mapenzi na kuepukana na uharibifu ambao utaiharimu Serikali kufanya marekebisho ya mara kwa mara ambayo yataondosha hadhi na uasili wake.
Halikadhalika, amewataka uongozi wa mradi huo wa Bustani ya Afrikan House ya Mji Mkongwe kuanzisha safari za baharini kuwapeleka wageni katika pembe yengine za kisiwa kama vile Nungwi na kwengineko, kupitia boti zitakazokuwepo katika mradi huu ili kutanua wigo katika sekta ya Utalii Nchini.
Hata hivyo, Waziri Harusi ameipongeza wizara na mamlaka za kiutalii kwa kuja na miradi muhimu ambayo yatasaidia kuendeleza utalii na kuporesha haiba ya Zanzibar.
''Mradi wa Bustani ya Africa House utakuwa sehemu muhimu ya maisha ya kijamii na kiutamaduni ya wakazi wa Shangani na wageni wa Zanzibar, pongezi ziende kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale,
"Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe pamoja na Kampuni ya Infinity kwa kuja na mageuzi makubwa katika nyanja za utalii kwa kuimarisha na kuanzisha vivutio vipya vya utalii nchini maana kwa muda mrefu kumeachwa nyuma katika harakati za kuboresha Utalii Zanzibar,'' amesema Waziri Harusi.