MANYARA-Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema Serikali imejidhatiti kurudisha hadhi ya Tanzanite kwa kufanya minada ndani na nje ya nchi ili kuyaongezea thamani na wafanyabiashara waweze kunufaika na kuongeza pato la taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 14, 2024 Mirerani mkoani Manyara wakati akizindua mnada wa madini ya vito ambao mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2017.
Mheshimiwa Mavunde amesema mojawapo ya maeneo yanayosaidia kuongeza mapato ni pamoja na kudhibiti biashara ya madini, kuzuia utoroshaji na kuifanya biashara hiyo kuwa katika mfumo sahihi, uwepo wa minada utachochea uongezaji thamani ya madini ya vito.“Madini ya Vito yananunuliwa kwa asilimia kubwa kwa ajili ya ‘luxury’ ni ufahari na madini ya vito tunashindana na watu wengine ndio maana Serikali inaendelea kuchukua hatua, tunarudisha hadhi ya Tanzanite ili ikashindane vizuri duniani,”amesema Waziri Mheshimiwa Mavunde na kuongeza,
“Moja ya hatua ya kwanza ni urejeshaji wa minada ya ndani na ya kimataifa, ili tuyape thamani madini yetu, duniani kuna madini mengi ya vito, moja ya sifa kubwa ya madini ya vito ni uadimu, Tanzanite ina sifa hizo; Ila sio madini pekee yake adimu, kuna nchi nyingine zina madini adimu ambayo hayapatikani popote hivyo tunashindana kimataifa ni lazima tuchukue hatua kuhakikisha tunarudisha hadhi ya Tanzanite katika soko la kimataifa ili na bei iweze kuongezeka na wafanyabiashara wanufaike,”amesisitiza Waziri Mavunde
Amesema, katika vipengele (category) vya mawe duniani, jiwe linaanzia kuwa Precious, semi-Precious halafu baadaye linakuwa jiwe la kawaida na kwamba wanachukua hatua za makusudi ili Tanzanite lisiwe jiwe la kawaida.
“Tukiacha liwe la kawaida mtanunua kwa kilo kwa gharama ndogo sana na mtashusha hadhi ya Tanzanite, Serikali haipo tayari kuona hilo linatokea ndio maana tunayafanya haya kwa ajili ya kuhakikisha tunalinda hadhi na heshima ya jiwe letu hili.” Amesisitiza Mheshimiwa Mavunde.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewahakikishia wadau wa madini kuwa Serikali haitachukua madini ya mtu baada ya mnada wa leo na kama kuna madini yatabaki yatakabidhiwa kwa wahusika.
“Kumekuwepo na hisia na dhana baada ya mnada Serikali itachukua madini yaliyobaki kwa sababu katika mnada wa mwisho wa mwaka 2017 kuna madini yalibaki na wahusika hawakurejeshewa mpaka leo, nataka niwahakikishie Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia kuhakikisha katika biashara hii pia tuwajengee ‘confidence’ mtafanye biashara kwa uhuru na hakuna namna yoyote kuwa serikali itawaingilia na kuja kuyachukua madini yenu.
“Yale madini yaliyochukuliwa yapo, yalibaki Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tumeshayatoa na tutawakabidhi rasmi wahusika ili waendelee na biashara yao ya madini, nataka niwatoe hofu na muwe na amani,”amesema Waziri Mavunde.
“Manyara tayari mna eneo ambalo tutajenga ‘Tanzanite Exchange Centre’ ambayo kwa sasa tumefanya mazungumzo na wadau tutajenga kitu kinaitwa ‘Tanzanite Smart City’ ambao utakuwa mji mkubwa wenye hoteli ndani yake, Helikopta ambazo zitatua humo humo, ukumbi mkubwa wa mikutano wahusika hivi sasa wapo Wizara ya fedha, likikamilika hili natamani siku moja mkutano mkubwa wa madini ufanyike Mirerani,”amesema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo ameongeza kuwa kupitia mnada huu uliozinduliwa leo, idadi ya wauzaji waliojisajili kwenye mfumo wa kielektroniki wa kuendesha minada ni 195 wakiwemo wafanyabiashara wadogo wa madini (brokers) 120, wafanyabiashara wakubwa wa madini (dealers) 59, waongeza thamani madini (lapidary) 7 na wachimbaji madini 9. Kiasi cha madini kilicholetwa kwenye mnada ni kilogramu 184.06 kinachokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 3.10.
Wakati huohuo akizungumza kwenye uzinduzi wa mnada huo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda amempongeza Waziri wa Madini kwa kuweka nguvu kubwa kwenye utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kuwezesha wachimbaji kuchimba bila kupoteza mitaji ikiwa ni sehemu ya “Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri,” na kuongeza kuwa,
“Kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini unakua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.”
Naye Mbunge wa Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka amepongeza jitihada za Serikali kwa kupania kuleta mapinduzi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, kuhakikisha dhahabu inanunuliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi.
“Ninashauri Serikali kuendelea kutilia mkazo wa biashara ya madini ya vito kuendelea kufanyika katika mji wa Mirerani wakati ujenzi wa Soko la Madini Mirerani ukiendelea” amesisitiza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara , Mheshimiwa Queen Sendiga ameongeza kuwa minada ya madini ya vito italeta manufaa makubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza kipato kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, serikali kupata mapato, kuimarisha ubora wa madini ya vito na kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini.