ZANZIBAR-Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema, majengo ya kambi ya Kikosi cha KMKM ndio kiungo muhimu cha kuhakikisha usalama wa bahari na kuwapatia misaada wananchi pale ambapo wanapotokezewa na majanga wakiwa baharini.
Akizungumza katika ufunguzi wa majengo hayo huko Kizimkazi ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 61 ya mapinduzi amesema, kikosi hicho kina wajibu wa kuhakikisha na kuendelea kupinga usafirishaji wa magendo, uvuvi haramu, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya na uharibifu wa mazingira na mali asili za bahari.
Pia,amewataka maafisa hao kuendeleza ushirikiano pamoja na wananchi na serekali kwa ujumla juu ya vitendo vyote ambavyo havikubaliki katika nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ,Issa Mahfoudh akisoma taarifa ya kitalamu alisema ujenzi huo umetumia zaidi ya shilingi milioni 500 ikiwa ni fedha za serikali.
Vilevile amesema ujenzi huo umejumuisha jengo la ofisi, hanga la wapiganaji, nyumba ya mkuu wa Kambi, jengo la walinzi lenye eneo la kuhifadhi mafuta, nyumba ya Ibada (mskiti) pamoja na jiko.
Nay Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Komandoo Azana Hassan Msingiri amesema, maendeleo yote hayo yanatokana na ushirikiano wa idara za SMZ pamoja na wizara zake.
Ni katika kuhakikisha kambi hiyo inaonekana katika taaswira nzuri huku ikiwa imeokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zilitakiwa kwenda kwa wakandarasi wa nje.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Muhammed Mahmoud amewataka maafisa hao wahakikishe nchi inakua katika hali ya usalama kwa muda wote.
Aidha,amesema ujenzi huo ni muendelezo wa kuzijenga na kuziwekea thamani kambi za kikosi hicho na kuondoa changamoto ya uhaba wa kambi na mahanga ya kulala wapiganaji wanaohudumu katika kambi hizo.
Ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Kambi ya KMKM Kizimkazi ulianza Februari 4,2024 na kumalizika Novemba mwaka huu na kutimiza ahadi za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kikosi hicho.