Serikali yataja sababu za mfumuko wa bei kubaki asilimia 3.0

NA GODFREY NNKO

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 umebaki katika asilimia 3.0 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 10,2024 jijini Dodoma na Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Dkt. Albina A.Chuwa ikiangazia fahirisi za bei za Taifa kwa mwezi Novemba,2024.

"Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024."

Dkt.Chuwa amebainisha kuwa,kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba,2024 kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024 kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula.

Pia,kupungua kwa mfumuko wa bei kwa bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2024.

Amesema,baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba,2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024 ni pamoja na ulezi kutoka asilimia 3.7 hadi asilimia 5.9.

Nyingine ni unga wa mtama kutoka asilimia 5.4 hadi asilimia 6.8, mikate pamoja na vyakula vingine vya kuoka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 11.1.

Tambi kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 2.5, kuku wa kienyeji kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia 8.4, kuku wa kisasa kutoka asilimia 17.1 hadi asilimia 18.0, nyama ya ng'ombe kutoka asilimia 12.2 hadi asilimia 16.0.

Dkt.Chuwa amesema, pia nyama ya mbuzi ni kutoka asilimia 9.4 hadi asilimia 10.8, samaki wabichi kutoka asilimia 4.7 hadi asilimia 9.2, dagaa wakavu kutoka asilimia 18.9 hadi asilimia 20.5, maharage kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 4.8 na kunde kavu kutoka asilimia 8.0 hadi asilimia 8.8.

Kwa upande mwingine, Dkt.Chuwa amesema,baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 ikilinganishwa na mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024 ni pamoja na nguo za wanaume kutoka asilimia 2.0 hadi asilimia 1.2.

Nguo za watoto kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 1.2, viatu vya wanaume kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 2.1,viatu vya watoto kutoka asilimia 2.0 hadi asilimia 1.6.

Vilevile, nishati ya kuni kutoka asilimia 24.5 hadi asilimia 15.7, mkaa kutoka asilimia 22.7 hadi asilimia 17.3, samani za nyumbani kutoka asilimia 3.0 hadi asilimia 2.4.

Jiko la umeme kutoka asilimia 3.1 hadi asilimia 2.6,bidhaa na huduma kwa ajili ya starehe, michezo na utamaduni kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 2.0.

Pia,huduma ya chakula na vinywaji kwenye migahawa kutoka asilimia 2.8 hadi asilimia 2.7.

"Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 2.5 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2024.

"Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba,2024 umepungua hadi asilimia 2.9 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2024."

EAC

Kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba,2024 Dkt.Chuwa amebainisha kuwa,nchini Uganda, Mfumuko wa Bei kwa umebaki katika asilimia 2.9 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2024.

"Nchini Kenya, Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024 umeongezeka hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 2.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2024."

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 ya kutoa,kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu Rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Mfumuko wa Bei kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau wa takwimu.

Aidha,Mfumuko wa Bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news