DAR-Serikali imetoa shukrani za dhati kwa kundi la Mabalozi la nchi za Afrika nchini kufuatia uamuzi wa kundi hilo kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi milioni thelathini na nane kwa shule tatu za Sekondari ya Jangwani, Sekondari ya Pugu na Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu ambazo zina watoto wenye mahitaji maalum.

Balozi Shelukindo alisema kuwa msaada huo wa Kundi la Mabalozi wa nchi za Afrika ni kitendo cha kupongezwa na ishara ya wazi ya kuonesha utu, huruma na mshikamano kwa watu wenye ulemavu.
"Hiki kitendo kimeonesha maana kamili ya kuanzishwa kwa Siku ya Kuadhimisha Watu Wenye Ulemavu ambayo inalenga kutukumbusha jukumu letu la kibinadamu la kuwasaidia watu wenye ulemavu,"Balozi Shelukindo alisema.
Balozi Shelukindo alieleza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya ngazi ya kimataifa, kikanda na ya hapa nchini inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imekuwa ikitekeleza programu tofauti kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanaishi vizuri.
