DAR-Vilabu vya Simba Sports Club ya jijini Dar es Salaam na Pamba Jiji FC ya jijini Mwanza zimepigwa faini ya shilingi milioni tano kila moja.
Ni kutokana na vurugu zilizotokea siku moja kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kati ya timu hizo iliyopigwa Novemba 22, 2024 katika dimba la CCM Kirumba.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 2, 2024 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Pamba Jiji FC imetozwa faini hiyo kwa kosa la maafisa wake kuingilia mazoezi ya Simba SC siku moja kabla ya mechi hiyo iliyomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa 1-0.
Aidha,SSimba SC imetozwa faini kwa kosa la walinzi wake kufanya vurugu na kuvunja mlango na kioo cha dirisha la ofisi ya meneja msaidizi wa uwanja wa CCM Kirumba.
Pia,inatakiwa kulipa gharama za uharibifu uliofanywa na walinzi hao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.