DAR-Simba Sports Club imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ken Gold katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msimbazi walianza mchezo kwa kasi huku wakifanya mashambulizi mengi langoni mwa Ken Gold katika dakika 20 za mwanzo, lakini walikosa ufanisi wa kutumia nafasi walizopata.
Leonel Ateba aliwapatia bao la kwanza dakika ya 34 kwa mkwaju wa penati baada ya kiungo mshambuliaji Awesu Awesu kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na kiungo mkabaji George Sangija.
Ateba aliwapatia bao la pili kwa kichwa dakika ya 44 baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na mlinzi wa kushoto, Valentine Nouma.
Kipindi cha pili waliongeza kasi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini lakini walikosa ufanisi wa kuzitumia.
Ushindi huu unawafanya kurejea kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufikisha alama 31 baada ya kucheza mechi 12.
Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema, anawaamini wachezaji wote ndio maana amekuwa akifanya mabadiliko mara kwa mara kwenye kikosi chake na wamekuwa wakimpa matokeo chanya.
Pia,Kocha Fadlu amesema, anafurahi kuwa na kikosi chake kamili kwa kuwa ratiba ya mechi zimekuwa zinafuatana kila baada ya siku mbili ndio maana amekuwa akifanya mabadiliko ya mara kwa mara.