KILIMANJARO-Mwenyekiti wa Simba Sports Club,Murtaza Mangungu ameuomba Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumthibitisha Rais Wallace Karia kuendelea kuwa rais wa shirikisho hilo awamu ya tatu.
Ametoa mapendekezo hayo Desemba 21, 2024 katika mkutano huo unaofanyika mkoani Kilimanjaro ambapo hoja yake imeungwa mkono na wajumbe akiwepo Rais wa Young Africans Sports Club (Yanga SC), Mhandisi Hersi Said.
“Mafanikio makubwa ambayo Rais wa TFF pamoja na kamati tendaji ya TFF yamekuwa ni sababu kubwa ya maendeleo ya mpira wa miguu katika nchi yetu.
"Sisi kama wana soka katika taifa hili tunajivunia sana uongozi wako Rais, tunajivunia utendaji wako.
"Tunajivunia uchapa kazi wako, lakini pia nafasi yako kama mlezi wa soka katika taifa letu nakupongeza sana.”
Aidha,Makamu wa kwanza wa Rais TFF, Athuman Nyamlani amesema, haiwezekani kupitisha suala hilo katika mkutano huo ambao sio wa uchaguzi.
Nyamlani amesema, hatua hiyo itakinzana na utawala bora wa taasisi hiyo na kuahidi kulifanyia kazi jambo hilo.