Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yapongezwa elimu kwa vitendo

DAR-Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwaendeleza wanafunzi wenye mawazo ya kibunifu ili waweze kufikia malengo yao na kutekeleza Mpango wa Vituo Atamizi, unaowawezesha wanafunzi kujiajiri, kuajirika, na kuchangia uchumi wa Taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb,) kwenye sherehe za Mahafali ya 22 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika Kampasi ya Dar es Salaam Viwanja vya Kurasini ambayo ni Makao Makuu ya Taasisi hiyo.

Bi. Omolo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu ili kukidhi ongezeko la udahili.

“TIA ni miongoni mwa Taasisi zilizowezeshwa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 58.1, kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususan ujenzi wa miundombinu ya kusomea na kufundishia,”alisema Bi. Omolo.

Aliwapongeza uongozi na watumishi wa TIA kwa kusimamia vizuri rasilimali fedha na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa umakini.
Aidha, Bi. Omolo aliwasisitiza Menejimenti ya Chuo kuhakikisha inaweka mipango madhubuti ili kuhakikisha miundombinu iliyopo kwenye Taasisi hiyo inatunzwa ili iweze kukaa muda mrefu na kutumika na watu wengi.

Akizungumza na Wahitimu, Bi. Omolo aliwasisitiza kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya kwa lengo la kujifunza, kujitangaza kibiashara, na kujipatia kipato kwa kuwa ni rasilimali yenye nguvu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu, Prof. Jehovaness Aikael, aliwaasa wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho kwa kuonesha uadilifu na ufanisi.

“Mafunzo mliyoyapata hapa yakawe chachu katika jamii zetu kwa kuwa sisi ni wataalamu hivyo mkaipeperushe bendera ya TIA kwa kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mbalimbali na sehemu za kazi ili kuleta mabadiliko katika jamii,” alisema Prof. Aikael.

Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. William Pallangyo, alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya Wanafunzi mwaka hadi mwaka hilo limechangiwa na kuongezeka idadi ya wanufaika wa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Prof. Pallangyo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza idadi ya wanufaika na kiwango cha mkopo kwa wanachuo wa TIA.

Aliongeza kuwa katika mwaka wa masomo 2024/2025, jumla ya wanachuo 12,263 wamenufaika na mkopo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 7.49 kiasi ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 35.9 ikilinganishwa na wanachuo 9,025 katika mwaka wa masomo 2023/2024, waliopokea jumla ya shilingi bilioni 6.14.
“Ninayo furaha kubwa kukufahamisha kuwa, mahafali haya yameambatana na kuanzishwa kwa Kampasi ya Nane, Mkoani Tanga”, alisema Prof. Pallangyo.

Alifafanua kuwa ni hatua muhimu inayotimiza dhamira ya TIA ya kufikisha huduma karibu na wananchi kupitia Kampasi zake zilizopo Kanda zote za Tanzania.

Prof. Pallangyo, alisema kuwa Kampasi hizo zenye jumla ya Wanachuo 31,084, zipo kimkakati katika Mikoa ya Dar es Salaam (Kanda ya Pwani), Singida (Kanda ya Kati), Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu usini), Mtwara (Kanda ya Kusini), Mwanza (Kanda ya Ziwa), Kigoma (anda ya Magharibi), Tanga (Kanda ya Kaskazini), na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news