TFRA yakoleza kasi Kampeni ya Kuboresha Kilimo cha Pamba

SHINYANGA-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea na kampeni ya "Kijiji hadi Kijiji, Shamba hadi Shamba," yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa pamba. Kampeni hiyo inayofanyika kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania (CBT) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), inalenga kuongeza uzalishaji wa pamba kupitia teknolojia bora za kilimo.
Wakulima kutoka Wilaya za Meatu, Kishapu, na Igunga wamepatiwa mafunzo ya kina juu ya kilimo bora cha pamba, yakiwemo matumizi sahihi ya mbolea mashambani.

Mafunzo haya yanahimiza kubadili mbinu za uzalishaji zinazotumika sasa kwa lengo la kuongeza mavuno na kuboresha maisha ya wakulima.
Akizungumza na wakulima wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa TFRA Kanda ya Ziwa, Bw. Michael Sanga, ameeleza kuwa, matumizi sahihi ya mbolea yanaweza kubadilisha hali ya uzalishaji wa pamba.

Amesema kuwa kwa wastani, wakulima wanaweza kuvuna kilo 200 za pamba kwa ekari, endapo watatumia mbolea kwa kiwango sahihi na kuzingatia mbinu bora za kilimo, ambapo mavuno yanaweza kufikia zaidi ya kilo 2,500 kwa ekari.

"Matumizi sahihi ya mbolea yataleta mapinduzi makubwa kwa wakulima wa pamba. Hii ni fursa ya kipekee ya kuboresha maisha yenu kupitia kilimo cha kisasa," amesema Bw. Sanga.
Aidha, katika mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa Udhibiti Ubora na Majaribio, na Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi, Bw. Swalehe Mkuwili, amesisitiza juu ya uzingativu wa matumizi sahihi ya mbolea kwa kuzingatia kiwango kinachohitajika kwa mmea wa pamba.

Aidha, wakulima wamepewa mafunzo kwa vitendo jinsi ya kuweka mbolea kwa usahihi, jambo lililosaidia kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya mbolea mashambani.

Kampeni hii ya TFRA imepokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa, huku wakulima wakiamini kuwa mbinu na maarifa wanayopata yataongeza mavuno yao na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
TFRA, kwa kushirikiana na taasisi za serikali, inaendelea kuwa mshirika muhimu katika mapinduzi ya kilimo cha pamba nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news