NA LYDIA CHURI
JSC DODOMA
TUME ya Utumishi wa Mahakama (JSC) imekabidhiwa jengo lake na Mkandarasi wa ujenzi, Kampuni ya CRJE (East Africa) LTD baada ya kazi ya ujenzi kukamilika jijini Dodoma.Jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama lililomalizika kujengwa jijini Dodoma.
Hafla ya kukabidhiwa kwa jengo hilo imefanyika jana tarehe 30 Novemba, 2024 kwenye kiwanja namba 3 Block D katika eneo la NCC, pembeni ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa jengo hilo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bw. Rickneville Mwanri aliishukuru Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd kwa kufanikisha kazi ya ujenzi wa jengo hilo la Tume ambalo amesema litabadili mazingira ya kazi na kuwa bora zaidi kwa watumishi wa Tume.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bw. Rickneville Mwanri akipokea alama ya ufunguo kama ishara ya kukabidhiwa jengo la ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Kampuni ya CRJE (East Africa) LTD Bw. Xie Xiang.
“Tume haijawahi kuwa na jengo lake tangu kuanzishwa kwake hivyo kujengwa na kukamilika kwa jengo hili ni hatua kubwa, naipongeza sana Serikali kwa kuwezesha ujenzi huu. Jengo hili sasa litakuwa ni chachu kwa watumishi kuongeza kasi ya utendaji kazi”, alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema kuwa kiwanja kilichotumika kujenga jengo la Tume kina ukubwa wa mita za mraba 9,590, na kina hati yenye namba DOM008194 iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2022. Aliongeza kuwa jengo hilo limegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.3 (14,300,000,000).
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bw. Rickneville Mwanri akipokea Cheti cha kukamilika kwa jengo kutoka kwa Architect Queen Mduma Wakati wa hafla ya kukabidhiwa jengo la ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jana jijini Dodoma.
Awali akikabidhi jengo hilo, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd Bw. Xie Xiang aliishukuru Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuiamini Kampuni yake na kuipa kazi kubwa ya ujenzi wa jengo hilo la Ofisi.
Naye Mshauri Mradi huo, Architect Queen Mduma aliishukuru Tume kwa kuwaamini kusimamia Mradi wa ujenzi wa Jenggo lake ambapo amesema kazi imefanyika kitaalamu na kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi wa majengo makubwa.
Kujengwa kwa jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma kunaweka historia kwa Taasisi hiyo kumiliki jengo lake la ofisi tangu kuanzishwa kwake.
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Tanzania pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya kukabidhiana jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama lililomazika kujengwa jijini Dodoma.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume hii imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.