MOROGORO-Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo rekebu kilichoanzishwa chini ya Kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (Marejeo ya Mwaka 2019) chenye wajibu wa kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa kuzingatia Sheria,Kanuni,Taratibu na Miongozo.
Majukumu ya msingi ya Tume yameainishwa katika Kifungu cha 10(1) cha Sheria hiyo na yamegawanyika katika maeneo makuu matatu (3) ambayo ni kama ifuatavyo:-
(a) Kutoa Ushauri;
(b) Urekebu;na
(c)Kusimamia Utoaji wa Haki.
Tume ilifanya Mkutano wake Na. 2 wa mwaka 2024/2025 kuanzia tarehe 02/12/2024 hadi 20/12/2024 katika Ukumbi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Manispaa ya Mji wa Morogoro, chini ya Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Mst.) Hamisa H.Kalombola na kupitia, kujadili na kuamua Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma yaliyowasilishwa mbele yake.
Katika Mkutano huo jumla ya Rufaa na Malalamiko 379 yaliwasilishwa na kutolewauamuzi katika mchanganuo ufuatao:-(i) Rufaa 98 na(ii) Malalamiko 281Katika rufaa zilizowasilishwa na kuamuliwa, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi ni:
-(i) Kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma;
(i)Kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo;(ii)Uzembe kwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo;na(iii)Wizi wa mali za Umma.
Aidha, katika Mkutano huo, Warufani 30 na Mrufaniwa 1 waliomba na kuruhusiwa kufika mbele ya Tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa walizowasilisha Tume.
Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishiwa Umma za mwaka 2022.
Vilevile, Tume ilipitia Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume kwa Robo ya Kwanza (Julai - Septemba) kwa mwaka 2024/2025 pamoja na Taarifa ya Mapendekezo ya Kamati ya Ushauri na Maboresho ya Mfumo wa Ukaguzi,pamoja na Taarifa ya Mgongano wa Maslahi.
Tume inaendelea kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuzingatia Sheria ili kujiepusha na vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa maadili, hali inayoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu au za kijinai.
Ni muhimu pia kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kuendelea kuzingatia Sheria wakati wa kushughulikia malalamiko na mashauri ya nidhamu ya Watumishi ili haki itendeke.