ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameisisitiza jamii kuwaanda watoto na vijana kwa Elimu ya Dini ya mapema ili kuwajenga kuwa raia bora wa baadaye.
Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Disemba 13,2024 alipofungua Zawiya ISHAAT AUSWAF NNABIYY iliyopo Pitanazako Mbalungini Wilaya ya Kaskazin B, Unguja.
Amefahamisha kuwa,kuwapatia elimu ya mapema vijana kunatengeneza Taifa bora na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Aidha, Alhaj Dkt.Mwinyi amewapongeza waumini wa dini ya Kiislamu wa eneo hilo kwa kujenga jengo zuri la Zawia.
Akizungumzia suala la amani Alhaj Dkt. Mwinyi amewasisitiza viongozi wa dini na wanasiasa kutumia majukwaa yao kuhubiri amani wakati nchi ikielekea katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Vilevile Alhaj Dkt.Mwinyi amewanasihi waumini kuendelea kuiombea nchi Amani, Mshikamano,Upendo na Umoja.
Ufunguzi huo wa Zawia umeambatana na Dua maalum ya Kumuombea Rais Dkt.Mwinyi na Taifa kwa ujumla na hatimaye Alhaj Dkt.Mwinyi alijumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu kwa Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mbalungini uliopo Pembezoni mwa jengo la Zawia.