Uganda yafuraishwa na utendaji kazi wa Maabara ya GST na masoko ya madini

NA SAMWEL MTUWA

IKIWA ni siku ya pili ya ziara ya Ujumbe maalum kutoka Wizara ya Nishati na Idara ya Maendeleo ya Madini nchini Uganda, ujumbe huo umefurahishwa na mifumo ya utendaji kazi ya Upimaji na Utambuzi wa sampuli za madini na miamba katika maabara ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo , Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda Mhandisi Irene Bateebe amesema kuwa kulingana na mifumo iliyopo hususan katika mpangilio kuanzia upokeaji wa sampuli za miamba na madini mpaka kwenye hatua ya utambuzi tumejifunza mengi na imekuwa faraja kwetu kwa sababu tulichokiona ni maendeleo makubwa.

Mhandisi Bateebe amefafanua kuwa nchini Uganda wanayo taasisi inayojiuhusisha na upimaji na tafiti za jiosayansi ambayo inaitwa Uganda Geological Survey (UGS) lakini kwa upande wa Maabara Tanzania imepiga hatua.

Akielezea kuhusu mada ya upatikanaji wa Ithibati ya kimataifa kwa maabara , Mhandisi Bateebe ameeleza kuwa Maabara ya UGS bado haijapata Ithibati katika Elementi yoyote ya madini lakini kupitia ziara hii tumepata uelewa mpana wa namna ya kuandaa taarifa na nyaraka sahihi ili kupata ithibati.
Kwa upande wa masoko ya madini, Mhandisi Bateebe amefurahishwa na mifumo ya masoko kwa jinsi inavyofanya kazi pamoja kuweza kutambua uhalisia wa madini yanayopelekwa sokoni ikiwa pamoja na wingi wa idadi ya masoko yanayofanya biashara ya madini nchini.

Awali, akiwakaribisha katika ofisi za GST , Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba ameuelezea ujumbe huo kuhusu mikakati mbalimbali iliyopo ya kuongeza idadi ya uchunguzi wa sampuli katika elementi za madini mkakati na madini adimu ikiwa ni mpango maalum wa kisekta kupitia maabara za GST.

Naye Mratibu wa Mipango ya Maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Uganda,Bi. Hope Kyarisiima ameipongeza Tanzania kwa kuweka misingi imara katika mnyororo wa thamani madini ambao unalenga kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo ili kuondokana na umasikini pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake , Mkuu wa kitengo cha Miradi na Utafiti kutoka taasisi ya Chemba ya Migodi nchini Uganda Kenneth Asiimwe amesema kuwa, Sekta ya Madini nchini Tanzania imepiga hatua kubwa hususan katika ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo kwenye maeneo mbalimbali kama mada za GST na STAMICO zilivyoonesha wakati wa kikao.

Asiimwe ameongeza kuwa wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kuendeleza sekta ya madini , kwasababu wanachimba kwa mfumo endelevu hivyo juhudi ziendelee kuwajengea uwezo kwa maendeleo ya taifa.
Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo umepata fursa ya kutembelea masoko ya madini mkoani Dodoma ili kujionea biashara ya madini inavyofanyika katika masoko .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news