Uganda yajifunza usimamizi na uendeshaji Sekta ya Madini nchini Tanzania

DODOMA-Imeelezwa kwamba kwa kipindi kirefu Tanzania imekuwa ikifanya mageuzi mbalimbali ya kimaendeleo latika mnyororo wa thamani madini inayojumuhisha hatua za Utafiti, Uchimbaji, Uchenjuaji, Mifumo ya Masoko pamoja na Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuendeleza na kushirikisha mifumo yote inayozunguka Sekta ya Madini nchini.
Hayo yameelezwa leo Desemba 3, 2024 na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba wakati akifungua kikao cha majadiliano baina ya Ujumbe kutoka nchini Uganda na Wataalam wa Wizara ya Madini na Taasisi zake jijini Dodoma.

Mhandisi Samamba amesema kuwa, Tanzania imekuwa ikifanya mageuzi katika vipindi tofauti tofauti mapema baada ya kupata Uhuru wake Desemba 9, 1961, ikijumuhisha masuala ya Utafiti, Usimamizi na Uendelezaji kupitia taasisi zake za GST, STAMICO, TGC, TEITI na Tume ya Madini.
Kikao hicho kilianza na uwasilishaji wa mada kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada kuhusu majukumu ya GST ikiwemo kufanya tafiti za madini katika mfumo wa jiolojia , jiokemia na jiofikia katika skeli mbalimbali ambazo zinaonesha viashiria vya madini kulingana na eneo husika.

Aidha , Dkt. Budeba alieleza kuwa majukumu mengine ya GST ni kuhifadhi wa taarifa zote za Jiosayansi nchini, kupima sampuli za madini na miamba katika maabara zake pamoja na kuratibu majanga ya asili kama vile matetemeko ya ardhi, maporomoko ya udongo.

Kwa upande wake , mwakilishi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Fredrick Mangasini ameeleza kuhusu mikakati inayotekelezwa na STAMICO kwa kushirikiana na makampuni ya uchimbaji madini kwa niaba ya serikali ikiwa pamoja na miradi ya utafiti mfano uchorongaji, usimamizi wachimbaji wadogo kwa kutoa mafunzo ya kitaalam ya namna bora ya uchimbaji madini.
Miradi mingine inayotekelezwa na STAMICO ni pamoja na uongezaji thamani madini, utengenezaji wa nishati kupitia mradi wa mkaa mbadala na miradi mingine ya kimkakati kupitia kampuni tanzu ya STAMIGOLD.

Naye, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asili Tanzania (TEITI) Mariam Mgaya, ameueleza ujumbe huo kuwa katika kuweka uwazi na uwajibikaji TEIT imekuwa ikitekeleza majukumu ya kuhakikisha kampuni zinazofanya shuguli za utafutaji na uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia zinaweka wazi taarifa za shughuli za kulingana na viwango vya taaasisi ya kimataifa ya Uhamasishaji wa Uwazi katika sekta ya uziduaji (EITI).

Mgaya ameongeza kuwa, jukumu lingine ni kuwajengea uwezo wananchi katika kutumia taarifa na takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa makampuni ya uziduaji nchini.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kwenye mnyororo wa thamani madini kuna aina mbalimbali za kodi ikiwemo ukusanyaji wa kodi ya mapato, kodi ya mrabaha na kodi ya ada za madini.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe kutoka Uganda Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda Mhandisi Irene Bateebe ameishukuru Wizara ya Madini nchini Tanzania kwa uzoefu walioutoa katika kuendeleza Sekta ya Madini na kuhaidi kuupeleka uzoefu huo nchini Uganda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news