ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uzinduzi wa ujenzi wa barabara za juu (Flyover) ni mwendelezo wa kukamilisha ahadi na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 ambayo imevuka malengo kwa mafaniko makubwa ya miradi ya maendeleo.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu (Flyover) ya kwanza Zanzibar kwa awamu ya mwanzo, Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni ufunguzi wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa ujenzi huo wa Flyover ni mwanzo wa mambo makubwa zaidi yanayokuja na kueleza Serikali inampango wa kujenga mradi mkubwa wenye makutano ya barabara nne za juu (Interchange Road) na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali yao.
Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi amewasihi wanasiasa, viongozi wa umma na binafsi kuwa na uongozi wenye kuacha alama kwa kuweka maendeleo ya historia kwa vizazi vya baadae.
Akizungumzia kaulimbiu ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar isemayo “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo yetu”, Rais Dk. Mwinyi amewasihi wananchi kuendeleza amani na mshikamano uliopo kwa lengo la kuiendeleza nchi kwa maendeleo.