Undugu wa Watanzania na Waganda utaimarishwa zaidi na bomba la mafuta-Balozi Mwesigye

NA DEREK MURUSURI

BALOZI wa Uganda nchini Tanzania, Col (Rtd) Fred Mwesigye, amewataka watanzania wachangamkie fursa nyingi za kiuchumi zinazoletwa na bomba la Mafuta la Uganda na kusema litaimarisha undugu.
Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu, Mhe. Fred Mwesigye (Kushoto) akiongea katika hafla ya kumpongeza kijana wa Mwekezaji wa Mgahawa wa Break Point, Daudi Machumu (Kulia) aitwaye Kelvin Machumu, baada ya kumaliza Shahada ya Kwanza ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Ardhi.

Balozi Mwesigye amesema kuwa bomba hilo ambalo pia litasababisha mabomba mengine ya gesi ya Tanzania na mafuta safi, yataendelea kuwaunganisha watanzania kuwa familia moja.

"Kama ndugu mlitusaidia kumuondoa kiongozi mbaya Uganda, Idd Amin, udugu wetu ukaongezeka, kwa kuwashukuru Mhe. Rais Museveni akasema hili bomba la mafuta litapita Tanzania na kudumisha udugu wetu zaidi kwa kuunganishwa na bomba la mafuta," alisema Balozi Mwesigye.

Amemtaka Mwekezaji wa Mgahawa wa Break Point, Bw. David Gamba Machumu, kwenda kuwekeza Kampala na pia kuleta nchini Tanzania chakula kinachopendwa Uganda cha matoke ili Waganda wanapokuja kutalii nchini Tanzania, wapate sehemu nzuri ya kula.

Balozi Mwesigye alihudhuria shughuli ya kumpongeza Bw. Kelvin Machumu, kijana wa Mwekezaji David Gamba Machumu, Mwekezaji wa Mgahawa maarufu wa Break Point, ambaye ametunukiwa Shahada ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi cha jijini Dar es Salaam.

BALOZI AMUASA KIJANA ASIHARAKISHE KUSOMA MASTERS

Balozi Mwesigye alimpongeza sana Kelvin Machumu na kumtaka asiharakishe kufanya Shahada ya Uzamili, yaani Masters ili apate uzoefu wa kazi kwanza.

"Kwanza fanya kazi hapa Break Point, ui-turn around [aibadilishe] biashara hii ya Mgahawa kwa vile wewe kwa sasa una maarifa na mbinu nyingi ulizosoma na kutafiti kutuzidi sisi," alisema.

Watanzania wanao mfano mzuri wa Mohamed Dewj (Mo), ambaye, baada ya kurudi kutoka Marekani alikokwenda kusoma, Baba yake alimkabidhi majukumu zaidi na kuibadilisha biashara yao, akaikuza biashara, ikaongeza mapato na faida ikaongezeka.
Mwekezaji David Machumu (kushoto), Kelvin na mwandishi wa habari hii, Derek Murusuri (Kulia) katika hafla ya kumpongeza Kelvin Machumu kwa kutunukiwa Shahada ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Ardhi.

Ushauri wa Balozi wa Uganda kwa Kelvin ulipongezwa na wahudhuriaji wengi kwa vile vijana wengi wanao unganisha Shahada ya Uzamili, wanakosa uzoefu utakaowasaidia kukosoa na kuboresha utendaji kazi kwenye tasnia waliyosomea na kupunguza kasi na ubora wa mageuzi katika utendaji kwa vile hawakupata fursa ya kutosha ya kufanya kazi na kuona mapungufu ili waje kuboresha.

WENGINE WALIOHUDHURIA

Mbali na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka aliongoza timu ya Viongozi wa sekta ya umma, wafanyabiashara mbalimbali maarufu jijini Dar es Salaam, Wanazuoni mbalimbali na ambao pia walihudhuria sherehe hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Bravo Coco Beach jana jioni.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dotto Biteko, Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe Anthon Mtaka pamoja na Wakuu wa Mikoa kadhaa, walikuwa miongoni mwa viongozi waliotuma salamu za pongezi kwa tukio hilo.

Mwekezaji Machumu aliwashukuru ndugu na marafiki waliohudhuria na waliotuma salamu za pongezi na heri kwa kijana wake Kelvin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news