Usiyoyafahamu kuhusu NHIF, ni zaidi ya huduma

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema, umeendelea kuimarisha na kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuhakikisha wanachama wake popote walipo nchini wanapata huduma bora bila usumbufu.
NHIF ambayo ipo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Irene Kisaka imekuwa miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma nchini ambayo yamefanyia kazi kwa vitendo maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kutaka mifumo ya Serikali iwe inasomana kidigitali.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alitoa maagizo hayo Aprili,mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini Desemba 5,2024 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Kisaka amesema,mifumo hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuondoa usumbufu wa wananchi kutembea na taarifa zao wanapohitaji huduma za afya.

"Sasa mgonjwa anaweza kupatiwa huduma popote, hata bila kitambulisho cha bima, kwani taarifa zake zinapatikana moja kwa moja kwenye mfumo."

Dkt.Kisaka amesema,NHIF imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya Sura ya 395 ambapo wanafanya kazi chini ya Wizara ya Afya.

"Mission yetu ni kuongoza katika huduma za afya Afrika na hata wiki iliyopita Jamhuri ya Gambia walikuja kututembelea kuona ni namna gani wanafanya kazi.

"Wao ndiyo wameanzisha NHIF ambayo ya kwao ina miaka miwili, kwa hiyo tumeingia makubaliano ya kubadilishana wataalamu watakuja walau kukaa huku na kujifunza.

"Lakini, mission yetu sisi ni kutoa huduma ya bima katika wigo mpana, lakini kutoa huduma bora."

Miongoni mwa kazi zao ambazo zipo kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa ni pamoja na kuandikisha wanachama.

Pia, kukusanya michango, kusajili vituo vya afya, kulipa madai kwa watoa huduma baada ya kutoa huduma kwa wanachama.

"Mfumo tunaotumia sisi ni fees for service yaani akishatoa huduma ndiyo analeta tunamlipa."

Aidha, amesema pamoja na kulipa madai pia huwa wanawekeza kiwango kinachobaki.

"Kwa hiyo hatuwezi kuwekeza kama bado tuna madai ya kulipa, kwa hiyo madai ni kipaumbele."

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, pia wanafanya Tathimini ya Mfuko mara kwa mara.

"Kwa sababu mfuko wetu una short term benefits,kwa hiyo tunafanya accurial evaluation na kutoa elimu kwa umma na hapa ninyi wahariri na wanahabari mnafit sana kwenye hilo eneo."

Wanachama

Katika hatua nyingine, Dkt.Kisaka amesema kuwa, wana wanachama wa aina mbalimbali ingawa wamewagawanya kwenye maeneo sita.

Eneo la kwanza amesema, ni wanachama ambao ni watumishi wa umma na lingine ni watumishi wa sekta binafsi.

Kundi lingine ni upande wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, madiwani, wanafunzi na pia wana vifurushi.

Vifurushi hivyo ni kwa wale ambao hawapo katika moja ya makundi tajwa.

"Wanachama wetu sehemu kubwa sana ni watumishi wa umma ambao ni asilimia 55, halafu tuna ambao wanatoka sekta binafsi ambao ni asilimia 14.

"Lakini, asilimia 26 ni wanafunzi na kwenye vifurushi wako asilimia tano.

"Lakini, hii tunatarajia itabadilika sana, mpaka mwezi Juni tunatarajia itabadilika sana kwa sababu tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote."

Vituo

Dkt.Kisaka amesema, kwa upande wa vituo vya afya, vingi ni vya Serikali ambavyo ni asilimia 73.

Kwa upande wa vituo binafsi, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, ni asilimia 18 ikiwemo asilimia 9 ambapo jumla wana vituo 10,004 nchini kote.

"Lakini hela nyigi zinaenda kwenye vituo binafsi kwa sababu ni vile vituo vikubwa vinavyotoa huduma kwa gharama zaidi."

Amesema, hadi Juni mwaka huu, mfuko umelipa madai ya shilingi 650.42 ambapo katika kiasi hicho asilimia 37 ililipwa kwenye vituo vya Serikali.

Kwa upande wa vituo vya madhehebu ya dini vimelipwa asilimia 28 kwa upande wa malipo.

Pia, amefafanua kuhusu madai ya kuna formula ambayo huwa inatumika ili kuangalia uhalisi wa madai.

"Kwa hiyo kuna wengine wanapita humo humo wanakuwa na madai ambayo siyo halisi...siyo sahihi.Kwa hiyo, yale yasiyofuata muongozo wa Serikali, lakini mengine ambayo wamezidisha hayo tunayaondoa.

"Ndiyo maana mnasikia hiyo rejection rate, kwa hiyo mtaona kwa Serikali katika madai yote ambayo tumeyapata kwenye vituo vya Serikali tulichowalipa ni asilimia 89.

"Kwa hiyo wao ni asilimia 11, lakini madhehebu ya dini asilimia 93 ina maana wao tumewapunguza asilimia saba tu. Na vituo binafsi, ni asilimia 91, kwa hiyo utaona kilichopungua ni asilimia 9 tu, japo wakikuyana na ninyi wanawaambia ni asilimia 18.

....wanatupiga asilimia 20, kwa hiyo nilitaka niweke hii ili muone kwamba saa nyingine taarifa zinazokuja zinaweza zikawa siyo sahihi sana."

NHIF

Kuhusu hali ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwa katika hali mbaya, Mkurugenzi Mkuu anakiri ingawa anabainisha kuwa,

"Ni kweli hali ilikuwa siyo nzuri kutokana na kwamba madai yalikuwa yanakuja juu zaidi kuliko kiwango cha michango."

Amesema, miongoni mwa visababishi ni pamoja na Toto Afya.

"Toka 2016/17 mpaka 2022/23 michango ambayo tulikuwa tunapata kutoka kwa watoto ni shilingi milioni 633.7 lakini wanatumia shilingi bilioni 2.274.

"Kwa hiyo unaona wanatumia asilimia 359 kwa huo mwaka. Mwaka 2020/21 Toto Afya ilichangia shilingi bilioni takribani sita, lakini wanatumia shilingi bilioni 40.6.

"Katika kila shilingi moja unatumia 600, kwa hiyo anatumia zaidi ya anachochangia.Pamoja na uhakiki na kila kitu na kuhakisha watu hawatumii kadi ovyo, utaona 2023 bado ilikuja ilafikia asilimia 313."

Amesema, hali hiyo inatokana na wengi wanaokata bima hiyo ni wagonjwa.

"Tayari ni mgojwa alikwishakwenda hospitali ameambiwa hapa gharama zake zitakuwa hizi, kanunue kadi ya bima ya afya.Kwa hiyo akishakata kadi ndiyo ndiyo anahudumiwa, na hii ndiyo imetusababishia matatizo makubwa.

"Kwa sababu akifanya hivyo anachukua malipo ya mwanachama mwingine kwa sababu kwenye bima mnachangia kapu moja, anayepata janga analipwa."
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, kwa kipindi cha miaka saba loss ratio ilikuwa asilimia 366.

"Na hiyo ndiyo ilitufanya tukasimama kidogo, lakini sasa tunakuja, si kwamba imesimama moja kwa moja, lakini inaendelea."

Toto Afya zitaendelea shuleni na vyuoni baada ya kuondoa sharti la wanafunzi kujiorodhesha na kufikia 100.

Ameeleza kuwa, kitakachohitajika sasa ni wazazi na walezi kusajili wanafunzi wao shuleni na watakaowahi watahudumiwa katika kipindi kilichowekwa.

Amesema, kitu kingine ambacho kimewaletea shida kwenye bima ya afya ni kulipa matibabu ya wastaafu ambao hawachangii.

"Pia, na yenyewe imekuwa ikienda ikiongezeka utaona kwamba tulianza na 151 tukaenda 152, lakini sasa imeendelea kukuwa.

"Hawa wastaafu walikuwa wanakwenda mara tatu kwa mwaka hospiltali, lakini ilikuja ikapanda mpaka anaenda mara saba kwa mwaka hospitali.

"Kwa hiyo unakuta, kwa mfano kipindi kipindi kinachoishia Juni 2024 tumelipa shilingi bilioni 91.6 kwa hiyo hii inakwenda kwa mtu ambaye hajachangia.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, kitu kingine ambacho kimesababisha hali hiyo ni magonjwa yasiyoambukiza.

"Kwa hiyo utaona kabisa kwamba magonjwa yasiyoambukiza gharama zimekwenda zikiongezeka kutoka asilimia 34 imekwenda mpaka 2024 asilimia 60 ya madai yote.

"Yaani madai yote ambayo tunalipa kwenye vituo asilimia 60 yanaenda kwa magonjwa yasiyoambukiza.

"Na hili ni eneo ambalo pia tunaomba sana kushirikiana kwenye kujenga awareness.Sasa hivi, vituo vingi sasa siyo tena wazee kwa sababu ingekuwa wazee tungekuwa na ile 91.

"Lakini,ukiangalia hapo magonjwa yasiyoambukiza tumelipa shilingi bilioni 371 kwa hiyo kama wazee ni 91 inamaanisha magonjwa yasiyoambukiza yanatoka kwa wazee tu."

Pia, amesema unywaji wa pombe ni miongoni mwa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza huku akitoa angalizo kwa wanywaji hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news