MOMBASA-Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judidhi Kapinga amesema uwekezaji uliofanyika kwenye Sekta ya nishati nchini Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu itazinufaisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Mashariki mwa Afrika (EAPP) katika biashara ya kuuziana na kununua umeme.

“Uzalishaji wa umeme awali ulikuwa kwa kiasi kikubwa ukitegemea gesi, lakini baada ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Julius Nyerere ambao kwa sasa unazalisha takribani megawati 1,175 tumekuwa tukitumia zaidi nishati ya maji kuzalisha umeme."
Ameongeza kuwa, Tanzania inazingatia suala la uzalishaji wa umeme kwa nishati mchanganyiko (energy mix) na kutoa wito kwa Nchi wanachama EAPP kuwekeza zaidi katika nishati jadidifu ambazo ni nishati safi.
Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa Tanzania ina mkakati wa kuhakikisha vijiji vyote 12,318 vinafikiwa na nishati ya umeme ifikapo 2025 na kuongeza kuwa tayari zaidi ya asilimia 99 ya vijiji vimeshafikiwa na nishati hiyo.
Kapinga ameeleza kuwa, Tanzania inatarajia kujiunga na mfumo wa kuuziana na kununua umeme wa Kusini mwa Afirka (Southern African Power Pool).
Amesisitiza kuwa, kwa Tanzania kuwa na miunganiko ya umeme ni muhimu na ndio maana kama inaungana na nchi tofauti tofauti katika biashara ya umeme ili kuufanya mfumo wa gridi kuwa imara.

