DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Mhe. Ridhiwani Kikwete ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuzingatia misingi ya ajira kwa wenye ulemavu.
Pongezi hizo amezitoa wakati akifunga mafunzo ya Watumishi wa Serikali, Mahakama na Taasisi za Umma yaliyodhaminiwa kwa ushirikiano wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Taasisi ya OSHA inayosimamia Usalama na Afya mahala pa Kazi, yaliyofanyika katika ofisi za OSHA jijini Dodoma.
Katika mkutano huo, Waziri Kikwete amewakumbusha umuhimu wa kuzingatia mafundisho waliyoyapata na kuendelea na mapambano ya kupinga unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu.
Waziri huyo wa Kazi amesema, ni jambo la heri kuona Mahakama inatoa kipaumbele kwa wenye ulemavu katika kada zote za kiutendaji ndani ya muhimili huo wa nchi.
Pamoja na salamu hizo Waziri wa Kazi aliwakumbusha watendaji hao hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha Haki na Maslahi ya Wenye Ulemavu yanasimamiwa kwa kutunga sera na mipango mbalimbali ikiwemo inayowezesha sera hizo kutekelezeka.