ZANZIBAR-Vijana na watoto wanaoishi na ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza (type 1) Zanzibar wamesema kuna,umuhimu wa jamii kufahamu maradhi hayo ili kutambua namna ya kuishi na kukabiliana na changamoto za wagonjwa hao.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa vijana wanaoishi na ugonjwa wa kisukari Zanzibar, Zuberi Abdalla, walipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha ikiwa ni sehemu ya ziara yao katika jiji hilo.
Alisema, kutokana na changamoto za maradhi hayo unahitajika uwelewa, uzoefu na ujasiri katika kumhudumia mgonjwa wa kisukari na kumsaidia kujitibu mwenyewe hata anapokuea mbali na uangalizi.
Kijana huyo alisema, watu wengi hawana ufahamu wa kutosha juu ya maradhi ya kisukari hasa kwa vijana jambo ambalo linasababisha kukosekana kwa huduma za kuwasiadia.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma alisema amejifunza mengi kuhusiana na ugonjwa huo hasa kwa watoto na kwamba umefika wakati kwa jamii kuwatambua watoto hao na kuwapa ushirikiano.
Alibainisha kuwa,mamlaka hiyo pamoja na kutekeleza majukumu yake ya kukusanya mapato kwa maendeleo lakini pia inathamini na kujali maendeleo ya jamii wenye uhitaji ikiwemo watoto wanaoishi na ugonjwa huo.
Awali kiongozi huyo alisema,Mamlaka ya Mapato itaendelea kuwa pamoja na vijana wenye ugonjwa wa kisukari ambao wameonesha uwezo wa kuwa mabalozi katika kulipa na kukusanya kodi kwa hiari.
Shuma aliwakumbusha vijana hao kuwahimiza wazazi wao kulipa kodi ili kuipatia Serikali fedha za kuendeleza miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo huduma ya afya.
Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu Wanaoishi na Kisukari ( DAZ), Haji Abdalla Ameir, alisema ziara ya vijana hao imelenga kuwajengea uwezo wa kujitambua, pamoja na uzowefu wa kuendelea kuishi na ugonjwa huo hata wakiwa mbali na uangalizi wa wazazi bila kuathiri hali zao za kiafya.
Alisema, pamoja na kutoa elimu kwa jamii vijana hao watapata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Arusha ikiwemo mbuga za wanyama ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuimarisha Afya ya akilli.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, Ofisa elimu ya watu wazima Sekondari katika jiji hilo, Ridhwan Ridhwan alisema ujio wa Vijana hao katika Mkoa huo kunaimarisha mashirikiano yaliyokuwepo kati ya pande mbili hizo na kwamba inaakisi kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo.
Ridhwan ambaye ni mwenyeji wa vijana hao alisema, jiji la Arusha limekua na mahusiano chanya na watu wa Zanzibar na wamekua wakishirikiana katika mambo mbali mbali ikiwemo elimu na michezo na kuwa ujio wa Vijana waoishi na changamoto za kisukari kumetanua mawanda ya mahusiano yao.
Alieleza kuwa,jambo la kufurahisha ni kuona watoto hao wanajitambua na kujikubali hadi kuweza kujitubu kwa kujipima na kujipiga sindano wenyewe kwa mujibu wa utaratibu bila kuhimizwa na kusimamiwa licha ya kuwa na umri mdogo.
Alisema, hali hiyo inawapa faraja wazazi na walezi kuona watoto wao wanakua salama hata wakiwa mbali nao.
Zaidi ya watoto 26 wanaoishi na ugonjwa wa kisukari Zanzibar na wahudumu wa afya wanne wanaendelea na ziara yao jijini Arusha kwa lengo la kutoa elimu ya maradhi ya kisukari na kuhamasisha utalii wa ndani.