*Yakabidhi msaada wa madawati 85 shule ya msingi Itumbi
MBEYA-Amani Mwasapile (si jina lake halisi) amekuwa ni mtoro wa shule kila mara, hii inasabishwa na yeye kutokupenda kukaa chini pindi awapo darasani, ukizingatia ukweli kwamba wilaya ya Chunya (anapoishi) kumekuwa na hali ya hewa ya baridi kila wakati.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Hatari na Utii wa Sheria wa kampuni ya Vodacom Tanzania Plc Agapinus Tax (pili kutoka kushoto) akimkabidhi madawati Afisa Elimu Wilaya ya Chunya, Melcdiades Kagande katika shule ya Msingi Itumbi jijini Mbeya. Timu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ya kampuni hiyo wamekabidhi jumla ya madawati 110, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya elimu nchini. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka Vodacom, Olaf Mumburi.
Lakini sasa Amani amefurahi kwamba madawati 85 yaliyotolewa msaada na kampuni ya Teknolojia na Mawasiliano ya Vodacom Tanzania ikiwa mkono kwa mkono na kampeni ya Twende Butiama inayotekelezwa na wadau mbalimbali ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo walioko Nyanda za Juu Kusini waliamua kuchanga kwa ushirikiano na wadau na hivyo kufanikisha ununuzi wa madawati hayo yaliyokabidhiwa katika shule ya Msingi Itumbi iliyoko wilayani Chunya, Mkoani Mbeya hivi karibuni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Itumbi, Amani Kasumbo alisema kwamba upatikanaji wa madawati hayo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.
“Tunawashukuru sana Vodacom kwa kufika hapa na kutuletea msaada wa madawati haya, kwa kweli hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza utoro wa masomo kwa wanafunzi wetu maana wengi wamekuwa wakikwepa kukaa chini muda wa masomo,” alisema Mwalimu Kasumbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Hatari na Utii wa Sheria kutoka Vodacom Tanzania Agapinus Tax alisema kwamba kampuni hiyo imekuwa ikiishi misingi ya Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere kupitia programu ya Twende Butiama ambayo wameshirikiana na wadau mbalimbali nchini.
“Mojawapo ya misingi hiyo ni elimu, ambapo sisi kama wadau tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunasaidia juhudi za serikali katika kuboresha elimu, na tunafanya hilo kupitia misaada mbalimbali ya kimiundombinu ikiwamo kuchangia madawati kama tulivyofanya hapa,” alisema Tax.
Kwa kipindi kirefu, kampuni hiyo kupitia asasi yake ya Vodacom Tanzania Foundation na wadau mbalimbali imekuwa mstari wa mbele kusaidia katika miradi ya elimu, afya, mazingira na ujumuishwaji wa kifedha.
Naye Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu wa Kampuni hiyo Abednego Mhagama aliongeza kwamba kampuni yao imeona umuhimu wa kusaidia katika eneo la elimu kwa vile ni mojawapo ya maeneo muhimu sana nchini.
“Hakuna nchi yoyote inaweza kuendelea bila kuwa na elimu bora, tunaishukuru serikali yetu kwa kulijali eneo hili, lakini nasi kama wadau, hatuwezi kubaki nyuma hivyo tukaungana na kufanikiwa kupata madawati 110 ambapo leo tunakabidhi haya 85 ambayo yatasaidia katika kupunguza tatizo la utoro shuleni hapa, maana sasa wanafunzi wengi zaidi watapata madawati ya kukalia wawapo madarasani.
Madawati yaliyosalia yatakabidhiwa mwanzoni mwa mwaka 2025 pindi yatakapokamilika,” aliongeza Mhagama.
Kampuni hiyo ya Teknolojia na Mawasiliano imekuwa ikishirikiana na wadau na asasi yakiwemo mabenki mbalimbali nchini katika kuendesha msafara wa Twende Butiama, unaohusisha waendesha baiskeli kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwamo nchi za jirani ili kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo wakiendesha baiskeli kutokea jiji la Dar es Salaam mpaka Butiama mkoani Mara huku wakigawa msaada wa madawati na kupanda miti katika maeneo ambayo msafara huo unapita.
Aidha, kabla msafara huo haujaanza, Vodacom kupitia asasi ya Vodacom Tanzania Foundation walianzisha harambee ya kukusanya fedha baina ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ambapo michango iliyokusanywa na timu ya Nyanda za Juu Kusini ndio imetumika kutoa msaada wa madawati katika shule ya msingi Itumbi.
Waendesha baiskeli wa msafara wa Twende Butiama kutoka mkoani Mbeya waliungana na kampuni ya Vodacom katika kukabidhi madawati hayo kama ishara ya ushirikano endelevu baina ya wadau hawa.