DODOMA-Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, ametoa rai kwa Vyama vya Ushirika Nchini kuwekeza katika Kuanzisha na kuvimiliki Viwanda ili sehemu kubwa ya Viwanda Nchini vimilikiwe na Vyama; ili Ushirika iwe ni Sekta inayoongoza kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana.
Ameyasema hayo Desemba 11, 2024 wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 29 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), uliofanyika jijini Dodoma.
Mhe.Kigae amesema kuwa katika kufanikisha hilo Serikali itaona uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi kwa mashine na vipuli vya mashine vitakavyo agizwa na Vyama vya ushirika kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao hapa hapa nchini.
Aidha, Mhe. Kigae amevihamasisha Vyama vya Ushirika kuwa na Program na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi katika maeneo yao na kuepukana na uharibifu wa Mazingira ikiwemo ukataji miti na kufanya kilimo kisicho rasmi kwani janga hilo ni kubwa na lina athari katika shughuli hasa za kilimo.
"Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, mnapaswa kushirikiana na Serikali na Vyama vya Ushirika kwa pamoja kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya Tabia nchi kwasababu shughuli nyingi za Vyama zinategemea mazingira,” ameeleza Kigahe.
Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Wanaushirika wapo katika hatua za mwisho kuanzisha Benki ya Ushirika ambayo itasaidia kutoa huduma za kifedha kwa vyama vyote vya Ushirika ikiwemo kutoa mikopo yenye riba nafuu.
Aidha, Dkt. Ndiege amesema kwa sasa sekta ya Ushirika imeendelea kuimarika, ambapo watanzania wengi wananufaika kwa kujiunga na vyama hivi nchini.