MTWARA-Kampuni za kuchakata taarifa za mikopo za Dun & Bradstreet na Credit Info, zimeelezea umuhimu wa watoa huduma ndogo za fedha kujiunga katika mfumo wa taarifa za mikopo ili kuboresha uwezo wa watoa huduma hao katika kufanya tathmini ya mikopo kwa usahihi na kupunguza mikopo chechefu.
Wataalam wa taasisi hizo wamesema hayo walipowasilisha mada kwa nyakati tofauti katika semina kwa washiriki kutoka kampuni za huduma ndogo za fedha Kanda ya Kusini, inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mtwara.
Akizungumza katika semina hiyo iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Afisa Maendeleo ya Biashara wa Dun & Bradstreet Tanzania, Bw. Brian Magai, amesema ni wajibu wao kusaidia taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) kuuelewa vizuri mfumo wa taarifa za mikopo, kushiriki na kutoa taarifa hizo kila wanapotaka kutoa mikopo.
“Faida zinazotokana na kutumia taarifa za mikopo kwa wakopeshaji ni pamoja na kudhibiti mikopo chechefu, kupunguza hasara na kuongeza mapato,” amesema.
Naye, Meneja Msaidizi wa Credit Info kwa upande wa taasisi ndogo za fedha, Bw. Emmanuel Matee, amezikumbusha kampuni zinazotoa huduma ndogo za fedha kwamba wana wajibu wa kutumia huduma zitolewazo na taasisi zao zinazochakata taarifa za mikopo ili waweze kuimarisha shughuli zao.

Aidha, wataalamu hao wameishukuru BoT kwa kuwaandalia fursa ya kukutana na wadau wao muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha nchini.

Benki Kuu imeandaa mfululizo wa semina kwa wadau wa sekta ya fedha kutoka Kanda ya Kusini, kuanzia tarehe 2 hadi 6 Desemba 2024, ili kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa taarifa za mikopo.