TANGA-Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema wananchi wa vijiji vya Manga hadi Mkata katika Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga watasherekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka 2024 wakiwa na majisafi na salama.
DAWASA kuanza kutekeleza agizo la Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso (Mb) alilolitoa kwa Mamlaka hivi karibuni la kuhakikisha inaboresha huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, DAWASA imepeleka vifaa ikiwemo mabomba ya inchi 6 ambayo yatatandazwa takribani kilomita 4.1 na vimepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Dkt.Batilda Buriani.
Mwakilishi wa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema mradi utatekelezwa ndani ya wiki tatu na ifikapo mwishoni wa mwezi Desemba, 2024 wakazi takribani 41,000 wa Manga na Mkata watanufaika na huduma ya Majisafi.
Naye Dkt.Buriani amesema DAWASA ni taasisi ya mfano na ya viwango vya kimataifa, hivyo ana imani mradi utatekelezwa ndani ya muda uliopangwa na wakazi wa maeneo ya Manga na Mkata watanufaika na huduma ya majisafi na salama.
"Tunamshukuru sana Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso kwa kutimiza ahadi yake na leo sote tumekuwa mashaidi kwa kupokea vifaa vya kuanza utekelezaji wa mradi," amesema Dk Buriani.
"Sasa maji Tanga ni Mwaa Mwaa, tunaomba katika utekelezaji wa mradi huu muwape kipaumbele vijana wa maeneo haya ya Manga na Mkata ambao ni wanufaika wa mradi huu, ili na wao wanufaike na uwekezaji huu," amesema Dkt.Buriani.
Mkuu huyo wa mkoa amesema“la mwisho niwaombe kama tulivyokubaliana Waziri kwa wananchi ambao hawatamudu kulipia gharama za kuunganishiwa, huduma kwa pamoja basi wapewe kwa mkopo wakulipia kidogo kidogo."
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando ameshukuru kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo na kuhaidi kusimamia ukamilike kwa wakati ikiwemo ulinzi wa miundombinu hiyo kuto kuharibiwa.
"Kijiji cha Manga ni moja ya Vijiji katika Wilaya ya Handeni vilivyowekea miundombinu ya maji mwaka 1974, wakati huo ulilenga kuhudumia wakazi 120,000 na sasa tuko zaidi ya wakazi laki nne."