DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) ameahidi kuwahudumia kimahitaji watoto wawili wa marehemu, Amani Kamguna Simbayao aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Simbayao alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Mifupa Muhimbili (Moi) jijini Dar es Salaam baada ya kushambuliwa na watu katika eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Disemba, 2024.
Dkt. Nchemba ametoa ahadi hiyo wakati akiongoza waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu katika Viwanja vya Michezo vya TRA, Kurasini jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maanry Mwamba ambaye aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Elijah Mwandumbya katika tukio hilo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuf Juma Mwenda kuhakikisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 200 kinatafutwa kwa ajili ya kuanzisha Mfuko Maalum utakaotumika kuwanunulia watoto hao (Najimu Amani Sumbayao (8) na Badria Amani Simbayao (3).
Sambamba na mama yao, Bi. Arafat Abdalla Ukomo, Hati Fungani za Benki Kuu ya Tanzania, kwa ajili ya uhakika wa kupata huduma stahiki kama vile elimu na mambo mengine.
Maelekezo hayo yanafuatia maombi yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila wakati akitoa salam za mkoa wake ambapo alipendekeza uwepo mpango mahsusi wa kuisaidia familia hiyo kimaisha ili iwe motisha kwa familia hiyo iliyopoteza shujaa aliyemwaga damu yake wakati akilitumikia Taifa.
Marehemu Amani Simbayao, alikuwa Afisa Usafirishaji (dereva) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambaye alipigwa na kuumizwa vibaya na watu akiwa kazini na wafanyakazi wenzake wengine wawili katika eneo la Tegeta Kwa Ndevu jijini Dar es Salaam wakati walipokuwa wakilifuatilia gari moja lililokuwa linashukiwa kukiuka masuala ya kiforodha.
Katika tukio hilo la kuuaga mwili wa marehemu, Mhe. Dkt. Nchemba alilaani vikali tukio hilo la watu kujichukulia Sheria mkononi na kumuua mtumishi asiye na hatia hata baada ya kujitambulisha kuwa ni Mtumishi wa TRA, na ametoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika na tukio hilo baya ili liwe fundisho kwa watu wengine.
Aliwatia moyo wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wasikatishwe tamaa na tukio hilo, bali waendelee kuchapakazi kwa bidii kwa manufaa ya Taifa.