DODOMA-Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kurejeshwa kwa Toto Afya Kadi kutaleta matumaini mapya na uelekeo thabiti wa Bima ya Afya hususan kwa kundi la watoto ambalo linahitaji uangalizi wa pekee.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo tarehe 17, Desemba 2024 jijini Dodoma, wakati akizindua vifurushi vitatu vya vya Bima ya Afya kikiwepo cha Toto Afya Kadi.
Waziri Mhagama amesema Mpango huo wa Toto Afya Kadi utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto za kiafya.

“Kila tunapokutana kwa ajenda ya ya Afya, tujue tunazungumzia usalama wa Taifa, maendeleo endelevu na uchumi wa nchi,” amesema Mhe. Mhagama.
Mbali na kifurushi cha Toto Afya Kadi kilichozinduliwa leo, vifurushi vingine ni Ngorongoro chenye huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga kuhudumia watanzania.
Waziri Mhagama amesema mara baada ya uzinduzi wa vifurushi hivyo ajenda iliyopo mbele ni ubora wa huduma, huku akiwataka watoa huduma kuibeba ajenda hiyo na kutoa huduma zenye tija kwa maslahi ya umma wa watanzania ili waone umuhimu wa Bima na ifikapo 2030 Tanzania iwe imetimiza malengo ya kidunia.

“Takriban vituo 9,826 nchi nzima, kati ya vituo hivyo, vituo 7,366 (sawa na 75%) ni vya Serikali, vituo 1,375 (sawa na 14%) vinamilikiwa na watu binafsi, vituo 1,006 (sawa na10.2%) vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na vituo 79 (sawa na 0.8%) vinamilikiwa na mashirika ya Umma. Vilevile kuna jumla ya kliniki 987 na Maabara 1,590”, amefafanua Mhe. Mhagama.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maagizo ya Bunge huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulisemea suala la Bima ya Afya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini Bw. Edga Gabriel amesema kuzinduliwa kutasaidia kutambua viashiria vya awali vya udanganyifu, hivyo wanaipongeza NHIF kwa ubunifu huo.