DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni Masauni ameahidi kusimamia utekelezaji wa katazo la kisheria la matumizi ya mifuko ya plastiki, usimamizi wa biashara ya kaboni ili kuongeza msukumo wa sekta hifadhi ya mazingira nchini.
Mhe. Mhandisi Masauni amesema hayo leo Desemba 13, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliyehamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Masauni amesema mwaka 2019 Serikali ilitoa maelekezo mahsusi kuhusu katazo la mifuko ya plastiki na kusema Ofisi hiyo itaongeza kasi ya usimamizi wa katazo hilo ili kulinda afya ya jamii,wanyama na mazingira.
“Tutashirikiana na Menejimenti ili kuhakikisha tunaongeza kasi katika kusimamia masuala ya katazo la mifuko ya plastiki, usimamizi wa biashara ya kaboni na utoaji wa vyeti vya tathimini ya mazingira (EIA) ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Waziri Masauni.
Kwa upande mwingine Waziri Masauni ameahidi kushirikiana na Menejimenti na watumishi wa ngazi zote ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo katika kuwahudumia wadau mbalimbali kupitia sekta za Muungano na Hifadhi ya Mazingira nchini.