MWANZA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza waongeze kasi ya ujenzi wa daraja la Simiyu lililoko wilayani Magu kwenye barabara kuu ya Mwanza-Musoma ili likamilike kwa wakati.Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 175, upana wa mita 12.3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa tatu, ulianza Oktoba 30, 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 29, 2025. Daraja hilo linaunganisha mikoa ya Mwanza na Simiyu.
Akizungumza na wananchi waliofika kwenye daraja hilo jana jioni Desemba 21, 2024, Waziri Mkuu alisema wilaya ya Magu ina fursa nyingi za kiuchumi na kukamilika kwa ujenzi huo, kutafungua milango kwa wana-Magu.
“Magu ni wilaya ya fursa kiuchumi, Magu ni pumulio la Jiji la Mwanza. Je wana-Magu mmejipangaje kuzikamata hizo fursa? Ninawasihi jengeni vituo vya mabasi, mahoteli, maeneo ya vyakula na burudani. Boresheni miundombinu ya usafirishaji ili mtu akitoka Mwanza awe na uhakika kuwa anaweza kurudi kwa haraka bila shida yoyote.”
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Katetula Kaswaga kutoka TANROADS Makao Makuu alisema mradi huo utakaogharimu sh. bilioni 48.7, unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.
“Mradi unajengwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) chini ya usimamizi wa mhandisi mshauri ambaye ni TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU). Kazi iliyofanyika hadi sasa imefikia asilimia 35,” alisema.
Mapema, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo, kutasaidia kupunguza ajali na msongamano kwa kiasi kikubwa kwani daraja la zamani lilikuwa na njia moja ila la sasa litakuwa na njia mbili.
Amesema ujenzi wa daraja la Simiyu ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini ambayo imelenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi. “Daraja hili lilijengwa kabla ya uhuru, lilikuwa limebakia peke yake kwenye barabara kuu za nchi nzima.”
“Serikali ya awamu ya sita ilishaamua kuondoa madaraja kama hayo kwenye barabara kuu nchini. Tungeliacha liendelee kuwepo, lingeleta changamoto ya foleni kwenye magari ya mizigo yanayokuja nchini na kwenda kupita kwenye daraja la Kigongo-Busisi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Sukuma katika kata ya Ng’haya ambalo linaunganisha wilaya za Magu na Bariadi.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 70, upana wa mita 11.3 na barabara unganishi za kilomita 2.3, linajengwa na mkandarasi mzawa ambaye ni Mumangi Construction Co. Ltd. Hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 24 na utagharimu sh. bilioni 10 hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema ujenzi wa daraja hilo ni utekelezaji wa moja ya mikakati ya Serikali ya kuboresha sekta ya miundombinu nchini na kwamba kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, na pia kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.
Alisema daraja litakapokamilika na barabara hiyo ikaanza kutumika, itafupisha safari za kwenda mkoani Mara. “Barabara hii itakuwa fupi sana, ni kilometa 74 tu kwenda Mara,” alisema.
Kwenye ziara hiyo ya siku moja, Waziri Mkuu alifuatana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba, Wabunge wa Magu, Sengerema, viti maalum na viongozi wa CCM mkoa wa Mwanza.