KIGOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Idara ya Menejimenti ya Maafa na Jeshi la Zimamoto kutumia mapendekezo yaliyomo kwenye tafiti ya marehemu Billy Mwakatage ambaye ni mhitimu wa shahada ya Uzamivu (PhD) aliyefanya utafiti kuhusu majanga ya moto kwenye masoko ya umma.
Ametoa wito huo leo Alhamisi, Desemba 05, 2024 alipomwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango kwenye mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Kawawa, Manispaa ya Kigoma. Shahada hiyo ilipokelewa na mjane wa marehemu Bi. Ningile Kapange.
Amesema kuwa, utafiti huo una mahusiano makubwa na shughuli inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa katika kudhibiti maafa na majanga mbalimbali.
"Kwa kuwa ameshahitimu na leo anapata shahada na amefanya utafiti wa kina kwenye eneo hili la maafa na hasa majanga ya moto ambayo wakati wote Serikali tumekuwa tukipambana nayo, msomi wetu marehemu Billy Mwakatage pamoja na utafiti ametoa mapendekezo mbalimbali, chukue utafiti huu na muufanyie kazi katika kukabiliana na majanga hapa nchini.”
Marehemu Billy Mwakatage wakati wa uhai wake alifanya utafiti kuhusu "Mambo Yanayoathiri na Nia ya Kuzuia Milipuko ya Moto katika Soko la umma nchini Tanzania”.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mpango wa mafunzo kwa wahadhiri nchini ili wapate fursa za kufanya utafiti kwa kushirikiana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Pia, ameiagiza wizara hiyo kuandaa mpango mahsusi wa kukuza kazi za ubunifu na iweke mkakati wa kuwezesha kuuza bunifu hizo. “Kama mnavyofahamu ubunifu ni biashara. Pia, ubunifu unazalisha ajira na kuongeza kasi yamaendeleo ya Taifa”