Waziri Mkuu awataka wafamasia kuzingatia maadili

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wafamasia nchini watoe dawa kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na waache kutoa dawa kiholela ili kuimarisha ufanisi wa huduma za afya na kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa yasiyo sahihi.
Ameyasema hayo leo Desemba 4, 2024 alipofungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama cha Wafamasia Tanzania, ambapo amewataka watumie ujuzi na utaalamu wao kuwapa wahitaji dawa sahihi na kwa kuzingatia vipimo na maelekezo ya Madaktari.

“Watanzania wenzangu, wakati umefika wa kuacha kutumia dawa pasipo ushauri wa watalamu wa afya. Nendeni katika vituo vya kutolea huduma za afya mpate vipimo na maelekezo sahihi ya matumizi ya dawa. Pia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba simamieni matumizi sahihi ya dawa hasa za antibiotics.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa suala hilo liende sambamba na kusimamia vizuri huduma za utoaji dawa katika maduka ya dawa na kuhakikisha madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya dawa na vifaa tiba yanadhibitiwa kwa ukaribu.

Aidha, Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba iongeze udhibiti wa upotevu wa dawa, hususan kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma.

“Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI tumieni mifumo iliyopo katika kuziba mianya ya upotevu dawa vituoni na upatikanaji wa maoteo sahihi ya dawa ili kuepuka dawa kuharibika.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutaja jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha huduma za dawa kuwa ni pamoja na kuendelea kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 16 kila mwezi kwa ajili ya dawa. “Hatua hiyo imeimarisha upatikanaji wa dawa hadi umefikia wastani wa asilimia 85.”

Waziri Mkuu amesema Serikali katika kuhakikisha nchi inaimarisha uwezo wa uzalishaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ambapo kwa sasa kuna viwanda 17 vya dawa, 75 vya vifaa tiba na viwanda 57 vya kutengeneza gesitiba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news