ARUSHA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awataka wahandisi wote nchini wazingatie miiko na maadili ya taalum hiyo ikiwemo kuitekeleza miradi ya ujenzi kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha halisi iliyotolewa.
“Sote tunatambua kwamba wapo wachache katika taaluma yenu ya uhandisi ambao wanaichafua kwa kufanya matendo ambayo ni kinyume na taaluma,lakini pia ni kinyume na maadili.
“Matendo hayo ni pamoja na rushwa, ubadhilifu, na ukosefu wa weledi. Hii si tu kwamba inachafua taaluma ya uhandisi, bali pia inaharibu taswira ya nchi.
Ameyasena hayo leo Desemba 06, 2024 kwenye Kongamano la Kimataifa la 14 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jijini Arusha.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Bodi ya usajili wa Wahandisi isimamie maadili ya kihandisi na makampuni ya kihandisi kwa mujibu wa sheria ili kulinda hadhi ya uhandisi nchini.
Waziri Mkuu ametoa rai kwa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) kuendelea kushirikiana na vyombo mbalimbali kuwabaini wanaokiuka maadili na sheria na kuchukua hatua stahiki kwani taaluma ya uhandisi ni muhimu na inapaswa kutunza na kulinda heshima yake.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mita na Usalama Barabarani kuhakikisha kuwa vizuizi na vituo vya ukaguzi vinazingatia usalama wa watumiaji na tahadhari zote za kiusalama.