ZANZIBAR-Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Riziki Pembe Juma amesema Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu ya Afya ili kuhakikisha inaimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto akiweka Jiwe la Msingi Nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Wilaya Pangatupu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamra shamra za kuelekea kilele cha kutimiza miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Wilaya Pangatupu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamra shamra za kuelekea kilele cha kutimiza miaka sitini na moja (61) ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema,katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020/2025 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu kwa kujenga majengo mapya zikiwemo nyumba za wafanyakazi pamoja na kuweka vifaa vya kisasa.
Waziri huyo amesema, CCM wakati wa Kampeni ya Uchaguzi wa Mwaka 2020 iliahidi na sasa Serikali inatekeleza ahadi ya CCM kwa vitendo kwa ajili ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya dharura ili kupunguza vifo visivyotarajiwa.
"Nimefarajika sana kuona kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kusimamia na kuhakikisha watoa huduma wa afya wanapatiwa makaazi mazuri ili kutoa huduma bora kwa wananchi."
Alieleza hatua ya Serikali kujenga makazi ya wafanyakazi karibu na hospitali inawapunguzia wafanyakazi masafa pamoja na kupunguza gharama za ufasiri za kuwafuata madaktari bingwa katika makazi yao.
Pia alieleza kuwa,nyumba hizo zinatarajiwa kuchukuwa familia kumi na sita (16) na kutoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Afya kuanza kufikiria utaratibu mzuri utakaoutumia ili kuzitunza nyumba ziweze kutumika vizuri ikiwemo kuzifanyia ukarabati kwa wakati stahiki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Matibabu, Dkt.Mngereza Mzee Miraji amesema,Serikali imejenga makazi ya wafanyakazi wa Afya karibu na hospitali ili kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kuwapunguzia masafa wafanyakazi wa hao.
Aidha, amesema mradi wa ujenzi huo umejengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ukikamilika unatarajiwa kugharimu takribani shilingi Bilioni 4 za Kitanzania na unajengwa na Mkandarasi Mazrui Bulliding Constructor na ulianzwa kujengwa Januari 2024 na unatarajiwa kumalizika Januari 2025.
Naye Mkuu wa Wilaya Kaskazini B, Juma Sururu Juma, Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuwajenge majengo hayo na kuwapelekewa miradi mengine ambayo inatekelezwa katika mkoa huo.
Pia amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu na kuiomba Serikali kuendeleza mradi wa ujenzi wa barabara inayo toka Bubwini, Pangatupu na Mahonda ikamilike ili Wananchi wa maeneo hayo waweze kutumia.